LIVE STREAM ADS

Header Ads

Taasisi ya FADev yawanoa Wahariri Kanda ya Ziwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Taasisi ya kuendeleza uchimbaji mdogo wa madini Tanzania (FADev) imekutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Kanda ya Ziwa kwa lengo la kujadili na kuweka mkakati wa kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuboresha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini nchini.

Taasisi hiyo imekutana na wahariri hao jijini Mwanza kupitia mafunzo ya siku mbili yaliyoanza Jumanne Agosti 30, 2022 katika ukumbi wa Hoteli ya Midland.

Akifungua mafunzo hayo, Katibu Mtendaji FADev, Theonestina Mwasha amesema yataimarisha ushirikiano wa pamoja na namna bora ya kukuandika habari zinazohusu sekta ya uchimbaji mdogo wa madini ili kuboresha sekta hiyo na kuwa na tija zaidi.

"Sisi ni wataalamu wa madini na nyie ni wataalamu wa habari hivyo tunashirikishana na kubadilishana uzoefu ili kwa pamoja tuweze kuisaidia Sekta ya uchimbaji mdogo kwa kuripoti habari sahihi ambazo zitaondoa dhana ya wachimbaji wadogo kuonekana bado wako kwenye hali mbaya ya kuharibu mazingira" amesema Mwasha.

Amesema wanaunga mkono jitihada za Serikali katika kutekeleza programu za kubadilisha uchimbaji mdogo ili uweze kutumia njia bora na salama ambazo zinalinda afya za wachimbaji wadogo pamoja na kutunza mazingira.

"Wachimbaji wadogo wamekuwa wakiharibu mazingira lakini wakifundishwa wanabadilika, tumekuwa tukiwasaidia kupata huduma za kitaalumu na kifedha kwa kuwapa elimu, kuwaunganisha na taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya kupata mikopo ili kujikwamua kiuchumi" amesema Mwasha.

Mwasha amesema taasisi ya FADev imekuwa ikiwasaidia wachimbaji wadogo kuimarisha shughuli zao na kuongeza pato la Taifa na kuboresha maisha yao wenyewe.

Kwa upande wake Meneja Miradi FADev, Evans Rubara amesema dhamira ya taasisi hiyo ni kuwa na ushirikiano wenye tija na endelevu na waandishi wa habari/ wahariri ili kusaidia kuikuza sekta ya uchimbaji mdogo wa madini nchini.

"Ninaamini mpango mkakati tutakao uweka utatusaidia kufanya kazi na nyie ili baada ya semina hii kuisha uwepo mwendelezo wa kuandika habari zinazohusu sekta ya uchimbaji mdogo wa madini" amesema Rubara.

Naye mwandishi wa habari na mwakilishi wa magazeti ya Serikali (TSN) Kanda ya Ziwa, Abela Msikula amesema mafunzo hayo yamempa chachu ya kuwatembelea wachimbaji wadogo wa madini kwa lengo la kujionea hali halisi ya utendaji kazi wao pamoja na changamoto zinazowakabili na hatimaye kuandika habari kwa weledi zaidi.
Meneja Miradi kutoka Taasisi ya FADev, Evans Rubara akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa waandishi wa habari kuandika habari zinazohusu sekta ya wachimbaji wadogo wa madini.
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya FADev, Theonestina Mwasha akifungua mafunzo kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Kanda ya Ziwa.
Baadhi ya wahariri Kanda ya Ziwa wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Wahariri kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wakifuatilia mafunzo hayo.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.