Luteni Kanali Mbanga: Mafunzo ya JKT ni nguzo muhimu ya kuandaa viongozi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Imeelezwa kuwa mafunzo ya JKT kwa vijana wa Tanzania ni nguzo muhimu ya kuandaa viongozi wazalendo, waadilifu na wenye uchungu wa Taifa kwani kupitia mafunzo hayo masomo mbalimbali hutolewa yakiwemo ya uraia.
Hayo yalibainishwa na Luteni Kanali Raphael Festo Mbanga Kamanda wa Kikosi cha JKT 834 Makutupora Septemba 20, 2022 Mjini Dodoma wakati akitoa taarifa ya mafunzo ya vijana kwa mujibu wa Sheria Operesheni Jenerali Venance Mabeyo mbele ya Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mwema wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.
Alisema vijana wanaopitia mafunzo ya JKT hufundishwa mafunzo mbalimbali kwa nadharia na vitendo baadhi ni uzalendo, uadilifu, utii na uhodari Unaojali kuzingatia misingi ya umoja na mshikamano wa Taifa.
“ Pia vijana hufundiswa maarifa mbalimbali ya ujasiliamali ya stadi za kazi hivyo tunaamini maarifa hayo waliyopata yatawasaidia kutambua fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao watakayoishi na kuzitumia kuinua uchumi wao na waTaifa kwa ujumla.” Alisema Luteni Kanali Raphael Festo Mbanga.
Luteni Kanali Raphael Festo Mbanga Kamanda wa Kikosi cha JKT 834. |
Aliongeza kusema kuwa mafunzo mengine ni ya awali ya kijeshi yanayowafanya
wawe majasiri, hodari na utimamau wa mwili hivyo wako tayari kutumika katika shughuli za ulinzi katika nchi pindi watakapohitaji.
Vilevile alisema kuwa kupitia mafunzo hayo yaliyochukua majuma 12 , vijana watakuwa na uwezo wa kutambua viashiria vya uvunjifu wa amani na usalama katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vinavyohusika ili vichukue hatua mapema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa JKT Col George Barongo Kazaula kwa niaba Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Ndugu Mabere alimshukuru Mhe. Mwema kwa kukubali mwaliko wa kufunga mafunzo hayo.
Alisema majukumu ya JKT ni malezi kwa vijana, kuzalisha mali na ulinzi wa Taifa na katika kutekeleza majukumu hayo JKT huwafundusha mafunzo vijana kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea.
“Kupitia mafunzo haya vijana hujifunza masomo ya darasani, masomo kwa vitendo, kazi za mikono na uzalishaji mali kwa lengo la kukuza moyo wa kizalendo, kuwajengea nidhamu, ukakamavu na ujasiri na hiyo itawafanya wajitambue kwamba wao ni sehemu ya jamii ya Watanzania wanaopaswa kuilinda, kuijenga, kuitetea na kuipenda nchi yao.” Alisema Col GB Kazaula.
Col George Barongo Kazaula Mwakilishi wa Mkuu wa JKT. |
Aliwataka wahitimu wa Mafunzo hayo kuwa tayari kulitumikia na kulilinda Taifa popote watakakuwa kwani wanafahamu dhana ya uzalendo, umoja, mshikamano, ukakamavu na kujiamini hivyo watumie elimu hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali pasipo kuvunja sheria za nchi.
Pamoja na hayo alisema Serikali inatambua na kuthamini umuhimu wa mafunzo ya JKT ndiyo maana imeendelea kuiongezea JKT uwezo wa kuendesha mafunzo hayo akiwaomba wakawe mabalozi wazuri waendako kwa kuelimisha jamii hasa wale ambao hawakupata nafasi hizo umuhimu wa vijana kushiriki mafunzo hayo.
Naye Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema alisema kuwa Serikali pamoja na malengo mengine lengo kuu la kuwaleta vijana katika mafunzo hayo ni kuwajengea Uzalendo na Mshikamano ili kuondoa Udini, Ukabila,Ukanda na hatimaye kuandaa vijana wenye maono chanya na Taifa ambao wanatarajiawa wawe viongozi bora siku za usoni,hatimaye Taifa liweze kusonga mbele.
“Kupitia mafunzo haya ni imani yetu na Taifa kwa ujumla kuwa mmejifunza Ukakamavu, Utii, Ujasiri, Stadi za maisha, Ujasiriamali pamoja na Ulinzi wa Taifa letu.” Alisema Mhe. Mwema.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema. |
Aliongeza kuwa Hakika mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwao binafsi na Taifa kwani wamekuwa Jeshi la Akiba ambapo wanaamini pindi Taifa litakapowahitaji kwenda kutoa msaada wataitikia wito na kwenda kulitetea Taifa popote pale kwa moyo na weledi mkubwa.
Alitoa wito kwa kwa vijana wanaohitimu kuwa mafunzo waliyoyapata yamewafanya wajifunze siri nyingi za Taifa na matumizi ya silaha, hivyo ni vema mafunzo hayo yakatumike kwa manufaa ya Taifa na kamwe isitokee kijana yoyote akarubuniwa na vikundi mbalimbali vya waasi ndani na nje ya nchi na kujiunga au kutoa siri za aina yoyote kwani tutaliweka rehani Taifa.
“Niwasihi sana Uzalendo mliojifunza ukaonekane kwa matendo yenu mema mbele ya jamii inayowazunguka na vijana wengine wajifunze kutoka kwenu.” Aliongeza Mhe. Mwema.
Kwa upande wao wahitimu hao vijana wa mafunzo kwa mujibu wa sheria walimuahidi Mgeni Rasmi kwamba watayatekelza kwa vitendo mafunzo yao na kuwa mfano bora kwa jamii wanayoiendea na wazazi wao kwa ujumla.
Na Maganga Gwensaga, Dodoma
Baadhi ya vijana wahitimu wa mafunzo ya vijana kwa mujibu wa Sheria Operesheni Jenerali Venance Mabeyo. |
No comments: