Shirika la Internews lawanoa viongozi wa Dini, Watendaji wa Kata na Wataalamu wa Afya
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Internews kupitia mradi wa Boresha Habari limetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini, watendaji wa Kata na wataalamu wa afya jijini Mwanza kwa lengo la kukuza mahusiano kati ya wadau na vyombo vya habari.
Akizungumza Alhamisi Oktoba 06, 2022 wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo ya siku tatu, Mkufunzi kutoka shirika la Internews Tanzania, Dotto Bulendu amesema yatasaidia viongozi hao kufanya kazi kwa ukaribu na vyombo vya habari na kuondoa ugumu ambao waandishi wa habari wamekuwa wakikutana nao pindi wanapohitaji taarifa.
Alisema moja ya changamoto ambayo wameiona ni namna ya kubainisha vyombo vya habari katika utoaji wa taarifa hivyo wametumia fursa hiyo kuwaelimisha juu ya kuita vyombo vya habari kulingana na aina ya maudhui ambayo wanahitaji kuyawasilisha.
"Vyombo mbalimbali vya habari vinautaratibu wake na miiko yake hivyo tumewapa elimu ya kuvitambua ili waweze kujua wanapokuwa na jambo la kutoa kwenye jamii wanatakiwa kuita vyombo vya habari ambavyo vinahusika na ujumbe huo ili uweze kufika kwenye jamii kwa urahisi" alifafanua Bulendu.
Bulendu alisema pamoja na kuwajengea uwezo pia amewashauri kuwa na maandalizi mazuri ya ujumbe ambao wanautoa kwa waandishi wa habari hatua itakayosaidia habari hizo kuchapishwa ama kutangazwa na vyombo vya habari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa warsha hiyo ambye pia ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli jijini Mwanza, Jacob Mutashi alisema amepata ufahamu wa mambo mbalimbali ambayo yatamsaidia kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na vyombo vya habari.
Mutashi alieleza kuwa amewahi kushuhudia usambazaji wa taarifa mbalimbali ambazo siyo sahihi hususani kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii, hivyo aliwaasa wananchi kutoamini kila habari wanayokutana nayo kwenye mitandao badala yake wajilidhishe kwenye mamlaka husika.
Naye Shekh Musabaha Haruna kutoka Kata ya Butimba jijini Mwanza alisema mafunzo aliyoyapata yatamwezesha kufanya kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mabatini jijini Mwanza, Lilian Noel alilishukuru shirika la Internews kwa kutoa mafunzo hayo, akisema mwanzo alikuwa hana uelewa juu ya kutoa taarifa kwa waandishi wa habari hivyo lakini sasa atashirikiana vyema na vyombo vya habari.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dotto Bulendu.
Viongozi mbalimbali jijini Mwanza ambao ni Shekh Musabaha Haruna kutoka Kata ya Butimba (kushoto), Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli Dkt. Jacob Mutashi (katikati) na Mtendaji wa Kata ya Mecco Imelida Chundu (kulia).
Mwakilishi wa Internews Tanzania, Rose Mwang
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa kwenye picha ya pamoja, jijini Mwanza.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
No comments: