LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanaume huwakacha watoto wasipoandikwa kwenye kadi za Kliniki- KIVULINI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto KIVULINI la jijini Mwanza limetoa rai kwa akina mama kuandika majina halisi ya baba wa watoto wao katika kadi za kliniki hatua itakayowasaidia kisheria watoto hao kupata stahiki zao ikiwemo mgawanyo wa mali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Yassin Ally aliyasema hayo Jumamosi Oktoba 08, 2022 wakati akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Ndoa na Mirathi kwenye kongamano la Jukwaa la Wanawake wa Ushirika (SACCOS) lililofanyika katika ukumbi wa Nyanza jijini Mwanza.

Ally alisema kumekuwa na changamoto kwenye mashauri mengi yanayowasilishwa katika ofisi za shirika hilo ambapo baadhi ya akina mama wajasiriamali waliopata watoto na wanaume ambao hawajafunga nao ndoa ama kuwatolea mahali huandika majina ya wajomba wa watoto hao kwenye kadi za kliniki na hivyo kusababisha mtoto kushindwa kupata haki zao ikiwemo jina halisi la baba pamoja na mahitaji mengineyo.

"Inapotokea mama anaanza kudai matumizi, baadhi ya wanaume wamekuwa wakitumia mwanya huo kuomba kadi ya kiliniki ili waone kama kweli jina lake ndilo limeandikwa, akikuta jina siyo la kwake hapo ndipo mgogoro unapoanzia na kusababisha baba kutomhudumia mtoto" alisema Ally.

Pia Ally alisema pamoja na ubize walionao wanawake wajasiriamali katika kutafuta kipato, wanapaswa kufahamu taratibu za kisheria kama Sheria ya ndoa na mirathi ili inapotokea wametarakiana na wenza wao, watambue hatua za kufuatilia ili kupata haki zao.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wa Ushirika (SACCOS), Magdalena Lwinga alisema lengo la kuaandaa jukwa hilo ni kuwajengea ujasiri wanawake kushiriki na kusimamia vyama vyao pamoja na kuhamasishana kujiunga kwa wingi kwenye SACCOS ili kujikwamua kiuchumi.

Awali akifungua jukwaa hilo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Mwanza, Hellen Bogohe aliwaomba wanawake hao kutumia vyama vyao vya ushirika kukopa mikopo inayotengwa na Halmashauri ili waendelee kukuza vyama vyao na kujiimarisha pia kiuchumi.

Alisema katika mikopo hiyo ya Halmashauri isiyokuwa na riba, warejeshaji wazuri na waaminifu ni akina Mama.

Sarah Urio ni mshiriki wa jukwaa hilo kutoka JUMAC SACCOS, alisema kupitia mada iliyotolewa ya Sheria ya Ndoa na Mirathi amejifunza ni kwa namna gani ataweza kupata haki zake endapo ndoa yake itaingia kwenye migogoro pamoja na kuwalea watoto kwa ukaribu ili kuondokana na vitendo vya ukatili.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Yasini Ally akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wa Ushirika (SACCOS), Magdalena Lwinga akizungumza kwenye kongamano hilo.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa Mwanza, Hellen Bogohe akifungua jukwaa la Kongamano la Wanawake wa Ushirika jijini Mwanza.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
Washiriki wakifuatilia kongamano la Jukwaa la Wanawake wa Ushirika jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.