LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kigogo Mwanza aingia matatani baada ya kujiunganishia maji kinyemela

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mmliki wa hoteli ya Tema iliyopo Mtaa wa Nyabulogoya Kata ya Nyegezi jijini Mwanza, ameingia matatani baada ya kudaiwa kujiunganishia maji kinyemela licha ya kusitishiwa huduma hiyo na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) tangu Januari 2021 kutokana na tuhuma za wizi wa maji.

Akizungumza Ijumaa Oktoba 07, 2022 baada ya zoezi la kukagua na kuondoa mabomba ya maji yaliyoungwa kinyemela, Mwanasheria wa MWAUWASA, Oscar Twakazi amesema walipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Nyabulogoya kwamba wanakosa huduma ya maji na baada ya kufuatilia walibaini mtuhumiwa huyo alijiunganishia maji kupitia miundombinu yao.

Twakazi amesema mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina la Ebeneza Foya alikuwa mteja wa MWAUWASA lakini alisitishiwa huduma ya maji kutokana na kuwa na malimbikizo ya madeni ya maji.

"Tuliwahi kumkamata lakini tulitumia Sheria ya Maji kumuadhibu ambapo alitozwa shilingi milioni moja na laki tano ambayo aliilipa. Tulifanya makisio ya matumizi ya maji ambayo yalifikia zaidi ya milioni mbili ambazo ziliingizwa kwenye akaunti yake kama deni la maji na hadi sasa fedha hizo hajazilipa" alieleza Twakazi

Twakazi alisema kutokana na hujuma hiyo, tayari wameshatoa taarifa katika kituo cha polisi Igogo na taratibu za kufungua kesi dhidi ya mtuhumiwa zinaendelea.

Kwa upande wake Mkuu Msaidizi Kanda ya Nyegezi upande wa mauzo na makusanyo, Stephen Otonde alisema mtuhumiwa huyo ana jumla ya akaunti tatu za mita za maji.

"Akanunti ya kwanza Jamal Awadh (Tema Hoteli 3) ambayo inadaiwa 90,950.50, akaunti ya pili ni Ebeneza Foya inadaiwa 907,467 na ya tatu ni John Foya inayodaiwa 78,490" alisema Otonde.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyabulogoya, Renatusi Manyanga alisema amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kukosa maji mara kwa mara hatua iliyomsukuma kufuatilia katika ofisi za MWAUWASA.

"Nilipeleka taarifa kwa Mkurugenzi MWAUWASA akaniahidi kuwa atatuma timu yake ili ije ifanye uchunguzi na leo nashukuru wamefika na wamejionea wizi wa maji unaofanywa hapa na kusababisha wananchi kukosa huduma" alisema Manyanga akitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa wanapobaini matukio ya aina hiyo.

Jitihada za kumpata mtuhumiwa huyo zilishindikana baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mafundi wa MWAUWASA wakiendelea na zoezi la kuondoa mifumo ya mabomba iliyounganishwa kiholela.
Mafundi wa MWAUWASA wakiondoa mifumo ya mabomba ya Maji iliyounganishwa kiholela.
Meneja Upotevu wa Maji MWAUWASA, Mhandisi Ramadhani Mramba akionyesha tenki linalotumika kuhifadhia maji yaliyounganishwa kinyemela katika Hotel ya Tema.
Mkuu msaidizi wa Kanda ya Nyegezi upande wa mauzo na makusanyo Stephen Otonde.
Mwanasheria wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mwanza MWAUWASA Oscar Twakazi.

No comments:

Powered by Blogger.