LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wiki ya Huduma kwa Wateja 2022, TANESCO Mwanza watua Metro FM

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2022, maafisa wa TANESCO Mkoa Mwanza wameendelea kuwafikia wateja kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari na kuwatembelea mitaani ili kutoa elimu kuhusiana na huduma zinazotolewa na shirika hilo.

Akizungumza Jumanne Oktoba 04, 2022 katika kipindi cha Pambazuko kinachorushwa redio Metro FM, Afisa Masoko TANESCO Mkoa Mwanza, Joyce Makori amesema katika kuboresha huduma kwa wateja, shirika hilo limekuja na mfumo wa CRM na kituo cha pamoja cha mawasiliano kwa lengo la kuwarahisishia wateja kuwasilisha changamoto zao kwa ajili ya utatuzi wa haraka. 

Makori amesema mfumo huo tayari umeanza kutumika kwa baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Dar es salaam na Pwani, na kwamba hivi karibuni utazinduliwa mkoani Mwanza ambapo utasaidia kuondoa usumbufu kwa wateja tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Naye Afisa Masoko TANESCO Mkoa Mwanza, Prisca Kayaga amesema katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2022, shirika hilo limeendelea kutoa elimu kwa umma ikiwemo kuhamasisha matumizi ya huduma ya kidijitali ya Ni-Konekt inayorahisisha mteja kuomba na kuunganishiwa umeme kwa muda mfupi zaidi.

Pia Kayaga amesema wanatumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuepuka kufanya shughuli za kibiashara katika miundombinu ya umeme ikiwemo chini ya nyaya za kusafirisha umeme mkubwa, transfoma, kuchoma moto maeneo yenye nguzo za umeme pamoja na watoto kutocheza kwenye waya wa kushikilia nguzo (stay wire).

Wiki ya Huduma kwa Wateja Duniani huadhimishwa kila mwaka wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Afisa Masoko TANESCO Mkoa Mwanza, Prisca Kayaga akitoa elimu kwa umma kupitia redio Metro FM.
Afisa Masoko TANESCO Mkoa Mwanza, Joyce Makori  akitoa elimu kwa umma kupitia redio Metro FM.
Maafisa wa TANESCO Mkoa Mwanza (kushoto) wakiwa kwenye mahojiano redio Metro FM.
Picha ya pamoja Maafisa wa TANESCO Mkoa Mwanza na watangazaji wa redio Metro FM.

No comments:

Powered by Blogger.