Serikali kuboresha Vituo vya Kulelea Watoto
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali ina mpango wa kuboresha Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi ili viwe na vituo maalumu na vya kisasa vya kulelea watoto wadogo wa wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo kupitia mpango wake maalumu wa elimu haina mwisho.
Hayo yamesemwa na Gloria Mufaeli mkufunzi mwandamizi kutoka wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wa kati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango wa serikali wa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliokatishwa masomo kupitia vyuo vya maendeleoya wananchi.
Bibi Gloria amesema kwa kuanzia katika vyuo vya maendeleo ya wananchi baadhi vyuo vina vituo vizuri vya kulelea watoto wadogo lakini pia serikali ina mpango wa kuviboresha zaidi vituo hivyo ili viwe na walezi wazuri pamoja na zana mbalimbali za kujifunzia watoto.
‘Tumegundua pia mabinti hawa wakija chuo na watoto wao wanakuwa na amani zaidi, wanaingia darasani na watoto wao wanawaacha kwenye kituo cha kulelea watoto na wakitoka masomoni wanawapitia na kwenda nyumbani’ alisema Gloria.
Aidha amesema mpango wa serikali ni kuhakikisha vyuo vyote vya maendeleo ya wananchi vinakuwa na vituo bora vya kulelea watoto wadogo kupitia pia wadau mbalimbali pamoja wakiwemo ESP kupitia program yao ya uwezeshaji kupitia ujuzi watahakikisha mtaala wa kuwafundishia watoto unaboreshwa, mazingira ya watoto yanaboreshwa pamoja na walezi kupatiwa mafunzoya kuwalea watoto.
Bibi Gloria amesema mpango huo wa serikali mbali na kuhakikisha wasichana hao wanapata elimu itakayowawezesha kufikia ndoto zao lakini umelenga pia kuhakikisha wasichana hao ambao waliokatisha masomo yao kutokana na ujauzito wanapatiwa elimu ya malezi na makuzi kwa mtoto.
"Wanapatiwa pia elimu ya kilimo cha mbogamboga ili familia zao ziwe na lishe bora lakini pia binti anapewa elimu ya malezi na makuzi ambapo mabinti hao huendana watoto wao ambao hulelewa katika vituo vya watoto wadogo vilivyoko kwenye vyuo hivyo vya maendeleo ya wananchi" alisema Bibi Gloria.
Kwa upande wake mshauri wa masuala ya kijinsia Dkt Alice Mumbi amesema kwa sasa ESP inaendelea na program ya mafunzo kwa wakufunzi kutoka vyuo vya maendeleo ya wananchi, asasi za kijamii, Ofisi ya Maendeleo ya Jamii pamoja na wizara ya elimu.
Dkt Alice amesemalengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki wa asasi hizo kupata mbinu mbalimbali zitakazo wasaidia kufanya mabadiliko chanya yatakayowezesha wanawake na wasichana kupata ujuzi wa fani mbalimbali na ujasiriamali kupitia Vyuo vya maendaleo ya wananchi na asasi za kijamii.
Na Tonny Alphonce, Mwanza
No comments: