LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanahabari wahimizwa kuelimisha jamii kuhusu magonjwa yasiyoambukiza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katika kuelekea kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza yatakayofanyika kitaifa mkoani Mwanza kuanzia Novemba 05-12, 2022, waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya ziwa wamepewa semina juu ya magonjwa hayo ili kusaidia kutoa elimu kwa umma.

Semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Afya imefanyika Jumatano Novemba 02, 2022 jijini Mwanza ikiwashirikisha takribani waandishi 50.

Akizungumza kweye semina hiyo, Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Shadrack Buswelu alisema lengo ni kuwawezesha waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza kwenye jamii ili kuwasaidia wananchi kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na magonjwa hayo.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Prof. Andrew Swai alisema magonjwa yasiyoambukiza yanaenea kwa wingi ikiwemo kisukari, Saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kuoza meno, magonjwa ya moyo, mishipa ya damu na magonjwa ya akili.

"Tafiti za mwaka 2012 zilizofanyika katika Wilaya 50 nchini, ugonjwa wa kisukari uliongezeka na kufikia asilimia Tisa, msukumo wa juu wa damu ulifikia asilimia 26, unene uliozidi ulifikia asilimia 34, kwa sasa dunia nzima asilimia 71 ya vifo vyote vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza na kwa Tanzania ni asilimia 34" alisema Prof. Swai.
Mwenyekiti wa vyama vya magonjwa yasiyoambukiza (TANCDA) profesa Andrew Swai akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya magonjwa yasiyoambukiza.

Prof. Swai alisema sababu za kuongezeka kwa magonjwa hayo ni mabadiliko ya mtindo wa maisha ikiwemo kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa, matumizi ya pombe, tumbaku, madawa ya kulevya, utawala duni wa msongo wa mawazo, kutopata usingizi wa kutosha, ajali au matukio yenye kusababisha majeraha mwilini, matukio ya ukatili, unyanyasaji, utelekezaji wa familia na majanga.

Kwa upande wake Debora Mpagama ambaye ni miongoni mwa waandishi waliohudhuria mafunzo hayo alisema elimu waliyoipata itawasaidia kuielimisha jamii ili kufahamu magonjwa yasiyoambukiza na umuhimu wa kufanya mazoezi ili kujiepusha na magonjwa hayo.
Wanahabari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wakifuatilia mafunzo hayo.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.