LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la TAHEA lazindua Jarida la Malezi ya Watoto

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Loata Molel (wa tatu) akizindua jarida la Mbeleko lililoandaliwa na Shirika la TAHEA ili kusaidia malezo bora kwa watoto.
***


Shirika la Uchumi wa Nyumbani (TAHEA) Mkoa wa Mwanza limezindua Jarida la Mbeleko litakalosaidia kutoa elimu kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla juu ya malezi bora kwa watoto ili waweze kukua katika maadili mazuri na kuwa raia wema.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu Disemba 12, 2022 kwenye Kituo cha Malezi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Mtaa wa Igombe, Kata ya Bugogwa, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza baada ya uzinduzi wa jarida hilo, Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Loata Molel amesema jamii inapaswa kuwekeza nguvu nyingi katika malezi na makuzi ya watoto kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kukua vizuri na kutimiza ndoto zao.

"Wazazi, walezi muda mwingi wameuwekeza kwenye utafutaji wa riziki kwenye suala la malezi ya watoto wamewaachia wafanyakazi wa nyumbani, nawasihi wazazi kuweka ratiba ya kusoma majarida mbalimbali yanayohusu malezi ya watoto likiwemo la Mbeleko ili waweze kuwalea watoto vizuri na kuwajengea misingi bora" amesema Molel.

Ameeleza kuwa Sayansi na Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa katika kujua mambo mbalimbali lakini pia imeleta changamoto kwenye malezi ya watoto kutokana na vitu vinavyokuwa vikioneshwa kwenye runinga hivyo wazazi wanatakiwa kuwa makini ili kuweza kuwanusuru watoto wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la TAHEA Mwanza, Mary Kabati amesema lengo la kuzindua jarida hilo ni kuendelea kuhamasisha jamii kuweka mazingira rafiki kwa watoto hususani kwenye malezi.

Amesema suala la malezi kwa watoto ni la muhimu sana lakini wazazi wengi hawana nafasi ya kukaa na watoto wao wala kujua maendeleo yao ya kimasomo.

"Ninaimani kupitia Jarida hili la MBELEKO wazazi na walezi watapata muongozo mzuri wa kuwalea watoto wao kwa kufahamu changamoto mbalimbali zinazoweza kuwapata pindi wanapokosa malezi bora" ameeleza Kabati.

Peter Matyoko ni Mratibu wa miradi ya elimu kutoka shirika hilo amesema jarida hilo linatumia mifano halisi ya utoaji malezi inayoonekana katika familia na jamii na kujaribu kukosoa, kusisitiza na kuboresha malezi hayo kwa kutumia simulizi ambazo zimetoka kwa watu mbalimbali.

Ameeleza jarida hilo limetumia vibonzo katika kuonyesha matukio yanayojitokeza katika familia na mitaani yanayohusiana na malezi ya watoto ili kuweza kufikisha ujumbe, kuongeza radha na kuwavutia wasomaji pia linatoa fursa kwa wazazi, walezi na jamii nzima kujadili na kutafakari juu ya malezi ya watoto kwa wakati huu ili kuchochea mabadiliko.

Anamaria Mwenge na Pastory Mswanzali ni miongoni mwa wazazi waliohudhuria uzinduzi huo, wamesema jarida la Mbeleko litawasaidia kujua mbinu mbalimbali za kuwalea watoto.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Loata Molel (katika) akionyesha jarida la Mbeleko baada ya uzinduzi.
Mkurugenzi wa Shirika la TAHEA Mwanza, Mary Kabati akizungumza kwenye uzinduzi wa Jarida la Mbeleko.
Mratibu wa Miradi ya Elimu kutoka Shirika la TAHEA Mwanza, Peter Matyoko (kushoto) akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu kuanzishwa kwa Jarida la Mbeleko. Kulia ni Mratibu Miradi ya Watoto TAHEA, Damas Joachim.
Baadhi ya wazazi waliohudhuria uzinduzi huo wakigawiwa jarida la Mbeleko.
Watoto pia wakishiriki uzinduzi wa jarida la Mbeleko. 

No comments:

Powered by Blogger.