LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mhandisi Sanga aridhishwa na mradi wa maji Tinde- Shelui

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi wa shilingi Bilioni 24.6 wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka kwenye Miji ya Tinde Mkoani Shinyanga na Shelui Mkoani Singida.

 

Mhandisi Sanga amedhihirisha hayo kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kukagua utekelezwaji wa mradi kwenye miji hiyo Januari 04, 2023.

 

Alisema Serikali inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha fedha za utekelezaji wa miradi ya majisafi na salama zinapatikana kwa wakati na hivyo kuwawezesha wakandarasi kutekeleza miradi hiyo kwa mujibu wa mikataba yao.  

 

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha fedha za utekelezaji wa mradi huu zinapatikana kwa ajili ya wananchi wa Tinde na Shelui,” alisema Mhandisi Sanga.

 

Akizungumzia hali ya utekelezaji wa mradi kwa ujumla wake baada ya ziara yake kwenye miji yote miwili, Mhandisi Sanga alibainisha kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi imekamilika kwa asilimia 99 kwa maeneo yote mawili kwani tayari maji yamefika kwenye matenki.

Alisema hatua inayofuata ni ujenzi wa mtandao wa kilomita 32 wa kusambaza maji kwenye miji yote miwili huku kila mji ukijengewa kilomita 16 za mtandao.  

 

Hata hivyo, alibainisha kwamba kwa upande wa Shelui tayari wananchi wameanza kutumia maji kutoka Ziwa Victoria kwakuwa wameunganisha kwenye mfumo wa usambazaji uliokuwepo tangu zamani na kwamba kinachofuata kwa Mji wa Tinde ni kuhakikisha maji yanasambazwa kwa watumiaji.

 

“Nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa, ninampongeza Mkandarasi Kampuni ya Megha Engineering and Infrastructure Ltd pamoja na Mtaalam Mshauri Kampuni ya WAPCOS Ltd kwa kukamilisha mradi huu,” alisema Mhandisi Sanga.

 

Alifafanua kwamba mradi wa kupeleka maji kwenye miji ya Tinde na Shelui unatoa maji kutoka katika mradi mkubwa wa Kahama-Shinyanga ambao pia umepeleka maji kwenye Miji ya Tabora, Igunga na Nzega.

 

Aidha, Mhandisi Sanga aliwapongeza wasimamizi wa mradi ambao ni Mamlaka za Maji za Shinyanga na Igunga kwa kushirikiana na Jumuiya za Watumia Maji Shelui pamoja na watendaji wa Wizara ya Maji wanaosimamia mradi huo moja kwa moja.

 

Vilevile aliwasihi watumishi wa Wizara ya Maji na Mamlaka za maji kuhakikisha miundombinu inalindwa na pia mazingira yanatunzwa ili kuwa na mradi endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Powered by Blogger.