LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mwanza kumaliza changamoto ya KKK kwa wanafunzi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wanafunzi 21,000 wa darasa la kwanza,la pili na la tatu katika shule za msingi za mkoani Mwanza ambao hawamudu kusoma,kuandika na kuhesabu (KKK)w anatarajiwa kuondokana na changamoto hiyo ifikapo mwezi wa tisa mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza Martin Nkwabi wakati akizungumzia hatua zilizofikiwa katika kuondokana tatizo la kusoma,kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la kwanza,la pili na la tatu.

Nkwabi alisema kuwa Desemba mwaka 2021 walikuwa na wanafunzi 37,000 waliokuwa hawamudu KKK,katika madarasa hayo lakini kwa kipindi cha mwaka mmoja wamepunguza idadi hiyo mpaka kufikia 21,000.

Akielezea njia waliyoitumia kupambana na tatizo hilo Nkwabi amesema walitafuta orodha ya watoto hao wenye changamoto ya kkk na kuwakabidhi Maofisa Elimu Kata orodha hiyo ambayo inataja jina la mwanafunzi,darasa na shule anayotoka ili wapewe mafunzo ya ziada yatakao wasaidia kuanza kusoma,kuandika na kuhesabu bila tatizo.

“Maofisa Elimu Kata tuliwaelekeza waweke mkakati maalumu kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi hao wanaweza kumudu kusoma,kuandika na kuhesabu,hatua hiyo ndio imewasaidia ambao wengine walioanzisha madarasa rekebishi,wengine waliamua kubadilisha walimu na kuweka walimu wengine huku wengine wanawafundisha kwa muda tofauti lengo ikiwa ni kuhakikisha wanafunzi hao wanapungua” alisema Nkwabi.

Alisema kuwa kila baada ya miezi miwili, wanatuma mtu anazifikia shule na kupima,ili kufahamu maendeleo ya watoto waliokuwa hawamudu KKK ili kupima kama idadi yao imepungua kwa kuwaita majina yao na kuwapima kwa kusoma,kuhesabu na kuandika.

Mbali na hilo ameeleza kuwa Walimu wanaofundisha darasa la kwanza na la pili ni wenye uwezo na wakifanya ufuatiliaji wakakuta Mwalimu Mkuu ameweka Mwalimu goigoi mwenye sifa mbaya darasa la kwanza na la pili,atakuwa amepoteza sifa za kuwa Mwalimu Mkuu.
Nkwabi alifafanua pia kuwa ufundishaji wa KKK unapita katika hatua kuu tatu,kwanza mwanafunzi anafundishwa kuandika hewani,akimudu kuandika hewani Mwalimu anamwambia twende ukaandike kwenye udongo hiyo ni hatua ya pili na akimudu anakwenda kwenye hatua ya tatu ya kuandika kwenye daftari lenye mistari mikubwa na midogo kisha akimudu katika daftari hilo ana hamia kwenye daftari lenye mistari ya kawaida.

"Tumegundua baadhi ya walimu wengine hawana uwezo wa kufundisha vizuri KKK kwaio tumewatafutia walimu wa kuwafundisha yani walimu wa kuwafundisha walimu wa madarasa ya chini ya la kwanza na la pili namna ya kuwafundisha wanafunzi hao chini ya programu ya Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini(MEWAKA)" alieleza Nkwabi.

Hivyo alieleza kuwa wanataka kila Kata iwe na kituo cha mafunzo hayo ili kuwajengea walimu uwezo ambao hawana uwezo mzuri wa kufundisha masomo yao na hii imewasaidia sana mfano Halmashauri ya Buchosa na Sengerema wamefanya vizuri sana katika programu ya MEWAKA, ambapo Mwalimu mwenye uwezo anamsaidia asiye na uwezo kuwa akitaka kufundisha fundisha namna hii ni mafunzo mazuri ambayo yameratibiwa na ofisi ya elimu.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamagana 'B' ,Theresia Silas akizungumza na mwandishi wa makala hii alipotembelea shuleni hapo, ameeleza kuwa katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu halmashauri ya Jiji la Mwanza imeweka utaratibu wa kuwapa mafunzo walimu wote wale wanahusika na KKK.

"Kama shule tupo kwenye utaratibu wa kuhakikisha kwamba wale wote ambao hawafahamu zile KKK wanazifahamu kwa ustadi unaohitajika kupitia juhudi za walimu na matumizi sahihi ya zana za kufundishia" alieeleza Mwalimu Theresia.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamagana'A' Anadoreen Rugaimukamu, ameeleza kuwa mpango wa kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili wanazifahamu KKK,kwanza ni wanao walimu wanaofanya kazi hiyo kwa madarasa hayo.

"Walimu wa elimu ya awali anapofundisha watoto,baada ya muda anakaa na wale ambao wanahitaji kuendelea kupata muda wa ziada kwa ajili ya KKK,na darasa la kwanza na la pili vilevile,yapo madarasa rekebishi ya awali Aidha yanatangulia darasa au baada ya darasa la kawaida,kwa ajili ya kusaidia wasiojua hizo KKK tunaimani kufikia Novemba tutakuwa na watoto wote wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu" alieleza Rugaimukamu.

Naye mmoja wa wananchi jijini Mwanza, Agnes Lucas alieleza kuwa katika kumaliza changamoto hiyo ya Kwa wanafunzi kutomudu KKK, wazazi washirikiane na walimu kwa kuhakikisha watoto wao wanaporejea nyumbani wanatenga dakika chache za kumfundisha kusoma,kuandika na kuhesabu.
Na Tonny Alphonce, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.