LIVE STREAM ADS

Header Ads

Bugando waendesha zoezi la upimaji bure magonjwa ya figo "ni kinyume cha sheria kuuza figo"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza imeadhimisha Siku ya Magonjwa ya Figo Duniani, kwa kutoa fursa kwa wananchi kufanya uchunguzi wa magonjwa ya figo ambayo asilimia kubwa yanatokana na mfumo wa maisha.

Akizungumza Machi 09, 2023 wakati wa kilele cha maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza, Dkt. Bahati Wajanga amesema wananchi wanapaswa kuzingatia mtindo sahihi wa maisha ikiwemo kufanya mazoezi, kupunguza uzito, kupunguza matumizi ya chumvi na kutumia dawa kwa usahihi kulingana na maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuepukana na hatari ya kupata magonjwa ya figo.

Amesema magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na presha yanachangia kwa asilimia kubwa ongezeko la wagonjwa wafigo na hivyo kuwahimiza wananchi kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi mara kwa mara kuanza matibabu mapema inapobainika kuna dalili za magonjwa ya figo.

Naye Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Figo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza, Dkt. Said Kanenda amesema changamoto ya magonjwa ya figo katika jamii ni kubwa ambapo kidunia kila wagonjwa 10 kati ya 100 wana changamoto ya figo.

Dkt. Kanenda amewaasa wananchi kuepuka matumizi yaliyopitilia ya pombe na sigara kwani yanachangia uwezekano mkubwa kwa mtumiaji kupata magonjwa ya figo. Ameongeza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya dawa ikiwemo za bakteria (Anti-Biotics) yanachangia magonjwa ya figo na hivyo kuwasihi wananchi kutumia dawa hizo kwa kuzingatia maelekezo ya daktari.

Amesema kuwa hospitali ya Bugando imekuwa ikitoa huduma za magonjwa ya figo ikiwemo dawa pamoja na usafishaji takamwili ambapo tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2023 wagonjwa zaidi ya 1,500 wamehudumiwa katika hospitali hiyo na kwamba kuanzia mwakani 2024 huduma ya kubadilisha figo inatarajiwa kuanza kutolewa hospitalini hapo.

Katika hatua nyingine Dkt. Kanenda amebainisha kuwa duniani kote ni kinyume cha sheria mtu yeyote kuuza figo bali hutolewa bure kama msaada kwa wahitaji hivyo wale wote wenye mawazo ya kuuza figo wanapaswa kuachana na mawazo hayo na kujikita kwenye shughuli halali za utafutaji kipato.

Baadhi ya wananchi walionufaika na huduma ya upimaji bure magonjwa ya figo akiwemo Becka Mugali na Ashura Hassan wamesema wakati mwingine wananchi wanashindwa kupima na kutambua mapema magonjwa ya figo kutokana na gharama hivyo fursa inayotolewa na hospitali ya Bugando kutoa huduma ya vipimo bure inawasaidia kutambua afya zao.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG 
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza, Dkt. Bahati Wajanga akizungumza na wananchi waliojitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa ya figo katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani 2023.
Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Figo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza, Dkt. Said Kanenda akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani yaliyofanyika katika viunga vya hospitali hiyo Machi 09, 2023 yakiambatana na zoezi la upimaji bure magonjwa ya figo.
Wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando wakitoa huduma kwa wananchi waliojitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa ya figo.
Wakazi wa Jiji la Mwanza waliojitokeza kupiga bure magonjwa ya figo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani 2023.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza waliojitokeza kupiga bure magonjwa ya figo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani 2023 iliyoambatana na kaulimbiu isemayo "Afya ya Figo kwa Wote, Tujiandae kwa Yasiyotarajiwa".

No comments:

Powered by Blogger.