LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanahabari wanawake Mwanza watoa msaada Kituo cha Nyumba ya Matumaini Nyegezi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa Mwanza kupitia uratibu wa MPC (Mwanza Press Club) wametoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika Kituo cha Nyumba ya Matumaini (House of Hope) kinachowasaidia watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Akizungumza Machi 19, 2023 wakati wa zoezi la kukabidhi msaada huo, Katibu Mkuu wa MPC, Blandina Aristides amesema lengo ni kuwakumbuka wazazi na watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ambao wanatoka katika mazingira magumu kiuchumi.

Aristides amesema msaada huo umejumuisha mahitaji mbalimbali ambayo ni pamoja na mchele kilo 100, sukari kilo 50, sabuni za mche boksi 10, mafuta ya kula Lita 40, juisi katoni 15 na mafuta ya kupaka mwili katoni mbili.

Naye Mratibu wa MPC, Laurancia Bernard amesema wanahabari wanawake jijini Mwanza wamewiwa kutoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake kulikuwa Machi 08, 2023.

Laurancia amewashukuru Waandishi wa Habari jijini Mwanza pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo EWURA, TIRA, NBC, Cecy Toto & Gift Shop na Jeshi la Polisi Mkoa Mwanza ambao wamefanikisha kupatikana msaada huo na kutoa rai kuendelea kuwa na moyo wa kuwasaidia watu wenye uhitaji.

Kwa upande wake Meneja wa Kituo hicho, Getruda Butondo ameeleza kufarijika na msaada huo akisema utasaidia kuwahudumia wazazi na watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa ambao hupokelewa kituoni hapo kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuhudhuria matibabu katika Hospitali ya Kanda Bugando.

Nao baadhi ya wazazi wa watoto wenye vichwa vikubwa akiwemo Mariam Habib kutoka mkoani Tabora na Janerosa Michael kutoka mkoani Geita wametoa shukurani kwa waandishi wa habari wanawake mkoani Mwanza kwa kutoa msaada huo na kuomba wadau wengine kuwaunga mkono.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG 
Meneja wa Kituo cha Nyegezi Nyumba ya Matumaini, Getruda Butondo (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa MPC, Blandina Aristes (kulia) wakati wa makabidhiano ya msaada huo.

No comments:

Powered by Blogger.