LIVE STREAM ADS

Header Ads

RC Singida ataka wananchi kulipa bili za maji kwa wakati

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu  wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (wa pili kushoto) na viongozi mbalimbali wakivuta pazia kuashiria uzinduzi 
wa mradi wa maji wa Kata ya Unyambwa uliogharimu zaidi ya Sh.Milioni 622 ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 6120 wa vijiji vya kata hiyo.

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amehimiza watumiaji wa maji kulipa ankara za maji kila mwezi bila kulaza ili kuiwezesha Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) iweze kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji, matengenezo na sehemu ya uwekezaji. 

Serukamba ameyasema hayo leo Machi, 17,2023 wakati akizindua  mradi wa maji wa Kata ya Unyambwa uliogharimu zaidi ya Sh.Milioni 622 ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 6120. 

Serukamba alisema wananchi mbali na kulipa ankara za maji kwa wakati pia wajiepushe na vitendo vya wizi wa maji kwani jambo hilo linaongeza mzigo wa gharama  kwa SUWASA na wateja wake. 

Aidha, Serukamba alitaja mambo mengine ambayo yataweza kuisaidia SUWASA kuwa ni kutunza vyanzo vya maji pamoja na miundombinu yote ya huduma, kutumia maji kwa uangalifu na kufuata taratibu zilizowekwa wakati wa kuomba maunganisho ya majisafi. 

Serukamba alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa wananchi wa Kijiji cha Unyambwa na uongozi wa kata hiyo hususani Diwani, Shabani Magwe kwa ushirikiano mkubwa ambao wameipatia SUWASA katika hatua mbalimbali za ujenzi wa mradi huo ikiwemo utoaji wa maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya maji na kuomba ushirikiano huo uendelezwe hata wakati wa uendeshaji wa mradi kwa kuwa Unyambwa sasa ipo ndani ya Manispaa na wananchi wanahitaji miundombinu ya majisafi iwekwe majumbani mwao.

Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA, Sebastian Warioba alisema mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya maji Kata ya Unyambwa, ni mradi wa awamu ya pili baada ya mradi wa awamu ya kwanza kukamilika mwaka 2018.

Alisema mradi wa awamu ya kwanza ulihusisha uchimbaji wa kisima eneo la Unyambwa juu na uligharimu kiasi cha Sh. Milioni  45.

Warioba alisema mnamo mwaka 2019, Watalaamu kutoka Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa kushirikiana na watalaamu kutoka SUWASA walikamilisha taarifa ya usanifu wa mradi wa maji katika Kata ya Unyambwa na taarifa iliwasilishwa Wizara ya Maji kwa maombi ya fedha za utekelezaji wa mradi huo na kuwa Wizaraya Maji kupitia Mfuko wa Maji (NWF) ilianza kutoa fedha za ujenzi wa mradi wa ujenzi miundombinu ya maji Kijiji cha Unyambwa mwaka 2021.

Aliongeza kuwa awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika kata hiyo ulianza Juni 1,2021 na ulitarajiwa kukamilika Septemba 01, 2021 na kueleza kuwa mradi huo haukukamilika kwa tarehe iliyokuwa imepangwa kutokana na fedha za mfuko wa maji kutolewa kwa awamu tofauti tofauti.

Alisema mradi huo umetekelezwa kwa kutumia watalaamu wa ndani wa SUWASA (SUWASA force account) na kuwa iwapo utekelezaji wake ungetumia utaratibu wa mkandarasi gharama ingekuwa zaidi ya Sh. Milioni  869.

Mwenyekiti wa Bodi SUWASA, Deocres Kamala alisema mradi huo utawasaidia watu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazolenga kuleta maendeleo katika Manispaa ya Singida, kama Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya maji mwaka huu inavyosema 'Kuongeza Kasi ya Mabadiliko Katika Sekta ya Maji kwa Maendeleo Endelevu ya Kiuchumi' na kuunga mkono jitihada za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru alisema mradi huo unakwenda kuwaondolea adha waliokuwa wakiipata wajawazito wakati wa kwenda kujifungua kwenye Zahanati ya kata hiyo kwani walilazimika kwenda na vidumu vya maji.


Mkuu  wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi huo wa maji. 
Mwenyekiti wa Bodi SUWASA, Deocres Kamala, akizungumza katika uzinduzi huo.
Kaimu Mkurugenzi, Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Richard Kasase akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA, Sebastian Warioba, akielezea mradi huo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru, akizungumza.
Wanawake wa Kaya ya Unyambwa wakiwakwenye uzinduziwa mradi huo.
Wanaume wakiwa kwenye hafla hiyo
Washiriki wa uzinduzi huo wakiserebuka wakati wakimsubiri mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Wanafunzi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akisalimiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Unyambwa, Ally Jingu.
Hafla ikiendelea.
Uzinduzi wa mradi huo ukiendelea. 

No comments:

Powered by Blogger.