WAZIRI MKUU APONGEZA TPDC KWA UJENZI WA SHULE YA MSINGI LIKONG'O KUPITIA MRADI WA LNG
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
📌Asema ni utimizaji wa majukumu ya kijamii kupitia miradi
📌Akumbusha shule kufungwa miundombinu ya Nishati Safi ya Kupikia kuunga mkono jitihada za Rais Samia
📌Mhe. Salome asema taasisi 52 zitasambaziwa nishati safi ya kupikia ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Mwigulu Nchemba amepongeza Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ujenzi wa shule bora ya Awali na Msingi katika Kijiji cha Likong'o mkoani Lindi inayojengwa kupitia mradi wa uzalishaji na usindikaji wa Gesi Asilia kuwa kimiminika ( LNG). .
Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo tarehe 20 Desemba 2025 wakati akikagua ujenzi wa shule hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 400 katika Kijiji cha Likong'o, Kata ya Mbanja, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.
" Nawapongeza TPDC kwa hatua hii ya kutekeleza shughuli za uwajibikaji kwa jamii (CSR) kupitia mradi huu wa LNG, shule hii ni bora ya kisasa na imezingatia mahitaji mbalimbali ikiwemo kuwa na miundombinu inayokidhi watu wenye mahitaji maalum na watoto wa kike." Amesema Mhe. Nchemba
Katika hatua nyingine Dkt. Nchemba ametoa msisitizo kwa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa shule hiyo inafungwa miundombinu ya Nishati Safi ya Kupikia kuunga mkono utekelezaji wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo kinara wake ni Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kutokana na uwepo wa shule hiyo, Waziri Mkuu amewaasa wananchi kuchangamkia fursa kwa kuwasomesha watoto wao na hivyo kuunga mkono jitihada anazofanya Rais Rais Samia za ujenzi shule katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha watoto wote kupata elimu.

Kwa upande wake Mhe. Salome Makamba ambaye ni Naibu Waziri wa Nishati, amesema mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Likong'o unatekelezwa kama sehemu ya kurudisha fadhila kwa wananchi waliotoa ardhi kwa ajili ya utekelezaji mradi wa LNG.
Ameeleza kuwa ujenzi wa Shule hiyo ambao umefikia asilimia 70 unaonesha jinsi kaulimbiu ya kazi na utu inavyotekelezwa kwa vitendo na Serikali ya Awamu ya Sita.
Katika hatua nyingine, Mhe. Salome ameeleza kuwa agizo la Waziri Mkuu la shule hiyo kuwekewa miundombinu ya nishati safi ya kupikia litatekelezwa na kuongeza kuwa ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan taasisi 52 zitasambaziwa miundombinu ya nishati safi ya kupikia.
Naye, Mbunge wa Lindi, Mohamed Utaly amemshukuru Rais Samia kwa uwekezaji huo wa mradi wa LNG ambao amesema unaleta chachu ya elimu mkoani Lindi.
Amepongeza pia TPDC kwa kuhakikisha kuwa miradi ya uwajibikaji kwa jamii imeanza kutekelezwa mapema kupitia mradi huo wa LNG.
Awali, Mhandisi Msimamizi wa mradi wa shule ya Awali na Msingi Likong'o, Upendo Mahavanu kutoka TPDC alisema mradi huo unagharimu Sh .bilioni 1.27 ambapo shule itakuwa na Madarasa 9; saba yakiwa ni ya shule msingi na mawili ni ya awali. Pia kutakuwa na ofisi na nyumba za walimu.
Utekelezaji wa mradi wa LNG unatarajiwa kuwa na manufaa mbalimbali nchini ikiwemo mapato ya Serikali yatakayotokana na uuzaji wa LNG kwenye soko la kimataifa, fursa za ajira, fursa kwa wazawa kuuza bidhaa, uhaulishaji wa teknolojia mbalimbali ili kuwajengea uwezo wataalam wa ndani n.k











No comments: