LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wadau: Serikali iboreshe mazingira kwa wenye mahitaji maalumu shule za awali na msingi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com

Wanafunzi wenye Ualbino wanahitaji zana bora za kujifunzia tangu wakiwa madarasa ya awali na msingi ili kuwa na msingi bora wa elimu. 

Na Abby Nkungu, Singida 

SERIKALI imeombwa kuangalia uwezekano wa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuweka miundombinu yote muhimu kwa watoto wenye mahitaji maalum katika shule zake za awali na msingi ili kuwezesha kutekelezeka kwa vitendo Sera ya elimu Jumuishi.

Chini ya Sera ya elimu Jumuishi ya mwaka 2014, watoto wenye ulemavu, wenye mahitaji maalumu na walio kwenye mazingira magumu wanatakiwa kusoma na wenzao wa kawaida kwenye shule moja bila kubaguliwa ili kila mtoto wa Kitanzania apate haki ya elimu bila kikwazo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadau wa elimu wanasema licha ya Sera hiyo kuwa mkombozi; hasa kwa watoto wasio na uwezo ambao  awali walikuwa wakifichwa majumbani kutokana na wazazi au walezi wao kushindwa kuwapeleka kwenye shule maalumu, changamoto ya kutokuwepo kwa mazingira rafiki kwenye shule Jumuishi bado ni kikwazo kingine.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linaloshughulikia maendeleo ya elimu Mtinko (MEDO), Iddi Hashim anasema kabla ya Sera ya elimu Jumuishi wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu na mahitaji maalumu walikuwa  wakilazimika kutafuta shule maalumu; ambazo hata hivyo ni chache.

“Sera hii imesaidia hasa kwa watoto wa chini ya miaka 8 maana  shule Jumuishi zipo jirani. Mzazi au mlezi anaweza kumpeleka mtoto wake  wa awali, darasa la kwanza au la pili shule mapema asubuhi kisha jioni akaenda kumchukua na kumrejesha nyumbani" anasema Iddi Hashim.

Hata hivyo,  Iddi anasema changamoto kubwa iliyobaki hivi sasa ni kwa Serikali kuongeza bajeti kwa shule hizo ili ziweze kuboresha mazingira ya kujifunzia na  kufundishia pamoja na kuweka miundombinu wezeshi kwa watoto wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu kusoma bila kikwazo.

“Hata wewe ungekuwa mzazi usingekubali kupeleka mtoto wako anatembea kwa mkono kwenye shule ambayo haina choo maalumu au mlemavu wa miguu kusikokuwa na  ngazi mtelezo au basi pale  Mtinko tulivyoona mtoto asiyeeona kwenye mtihani analazimika kusubiri mwenzake anayeoona amalize kwanza ndipo aanze kumsomea yeye” alisema na  kuiomba Serikali kuangalia suala hilo.

Anasema kuwa ingawa Serikali hivi sasa imekuwa ikihakikisha shule mpya za msingi zinakuwa na ngazi mtelezo na vyoo kwa wenye mahitaji maalumu, majengo ya zamani bado ni kikwazo, uhaba wa walimu wa elimu maalumu na zana za kujifunzia na kufundishia kama  vile maandishi ya nukta nundu, lugha ya alama, miwani kwa wenye uoni hafifu na mengine mengi. 

Mmoja wa wazazi ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii mstaafu, Patrick Mdachi anasema kuwa ingawa Sera ya elimu Jumuishi imesaidia; hasa watoto wadogo wasioweza kutembea umbali mrefu  kufuata shule za vitengo maalumu lakini bado kuna umuhimu kwa Serikali kuongeza bajeti ili ziweze kutekeleza kwa vitendo Sera hiyo na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

“Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ( PJT-MMMAM) iliyoanza Januari mwaka 2021 na inaendelea, inaangalia zaidi suala la elimu, afya, lishe, ulinzi na usalama wa mtoto; hivyo ni vizuri na  hii  Sera ikawekewa mazingira mazuri ili iweze kutekelezeka vyema” alisema na kuongeza kuwa lengo ni mtoto mwenye mahitaji maalumu kupata elimu bila kikwazo.

Msisitizo  wa wazazi  wengine, akiwemo Daudi Lameck mkazi wa Mtipa, Kulwa Ali wa SIDO na Neema Daniel  wa Sabasaba ni kwa Serikali kuboresha zaidi shule zinazotekeleza Sera hiyo ili kuvutia watoto hao.

“Zamani, wazazi na walezi tulikuwa tunawaficha hawa watoto majumbani ili wasisome, sio kwa kupenda bali tulikuwa tukiona akienda shuleni ni kama atateseka zaidi kulingana na mazingira yasiyo rafiki huko kuliko kubaki nyumbani lakini sasa hivi tunawatoa wakasome.....Serikali itusaidie kuweka mazingira mazuri” anasema Neema huku akiungwa mkono na Daudi pamoja na Kulwa.  

Takwimu za halmashauri ya Manispaa ya Singida  zinaonesha kuwa jumla ya watoto 84 wenye mahitaji maalumu wamesajili kwenye shule na vitengo mbalimbali kuanza masomo ya awali na msingi mwaka huu 2023 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka jana 2022.

Afisa elimu msingi katika Manispaa hiyo, Omary Maje anasema pamoja na sababu nyingine, mafanikio hayo ya uandikishaji watoto wenye mahitaji maalumu yametokana na utekelezaji mzuri wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya mwaka 2021.

Maje anasema chini ya Programu hiyo, pamoja na mambo mengine ya usalama, ulinzi, makuzi, afya, lishe na masuala mengine mengi mtambuka, viongozi na watendaji wa mitaa wamekuwa wakizunguka kwenye maeneo yao kuwabaini watoto hao na kutoa elimu juu ya umuhimu wa kupewa elimu.

Zana bora za kujifunzia kama hii anayotumia kijana huyu ni muhimu kwa watu wenye uoni hafifu.

Mfano wa choo bora kwa ajili ya matumizi ya wenye mahitaji maalumu pamoja na wengine wasio na mahitaji maalum.


No comments:

Powered by Blogger.