LIVE STREAM ADS

Header Ads

Jumuiya ya Wazazi Mabatini Mwanza yafikisha elimu ya maadili kwa wanafunzi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mabatini jijini Mwanza imeadhimisha Wiki ya Wazazi kwa kutoa elimu kuhusu mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtoni iliyopo Mabatini.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika Aprili 26, 2023, Katibu wa Jumuiya hiyo Kata ya Mabatini, Haji Said amesema vijana wengi wamekuwa wakiiga utamaduni wa kigeni hali inayopelekea kuwa na Taifa lisilo na maadili mema hivyo kutoa elimu kuhusu maadili itasaidia malezi na makuzi bora kwa vijana.

Said amesema wanajamii kwa kushirikiana na walimu wanapaswa kushirikiana na kuwalea vyama watoto ili kukomesha mmomonyoko wa maadili pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo vimekuwa vikiripotiwa katika jamii.

"Yale tunayoyaiga ndiyo yanasababisha mmomonyoko wa maadili, kuna msemo unasema mkataa kwao ni mtumwa na sisi tunaona tunataka kuwa watumwa, sasa kabla hatujawa watumwa tumeamua kukutana hapa ili kujadili usalama wa familia zetu" amesema Said.

Katibu wa Elimu, Malezi na Mazingira Jumuiya ya Wazazi Kata ya Mabatini, Magabe Mahelesi amesema wazazi wamesahau majukumu yao juu ya watoto na kutumia muda mwingi katika shughuli zao na kusababisha watoto kuingia katika vitendo viovu.

"Muda mwingi watoto wanajilea peke yao na sisi tumesahau majukumu yetu yanayotupasa ambapo hali hiyo inasababisha watoto kujipangia majukumu wenyewe na hatimaye wanaharibika kimaadili" amesema Mahelesi.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Kituo cha Polisi Wilaya ya Nyamagana, Kagemlo Muhula amesema mmomonyoko wa maadili unasababishwa na baadhi ya wazazi kushindwa kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto ipasavyo.

"Watoto wanaachiwa kujilea wenyewe, wazazi wanakuwa na visingizio vya kutafuta maisha na kushindwa kuangalia mwenendo wa tabaia za watoto wao" amesema Muhula.

Muhula amesema pia jamii inapaswa kuendelea kuripoti vitendo vya ukatili ili serikali kuendelea kuchukua hatua kwa watuhumiwa.

"Wakati mwingine inakatisha tamaa, mmemkamata mtuhumiwa na kesi imeendaa kwa mwanasheria na shitaka limetoka kesi imeendaa mahakamani, unashangaa mtuhumiwa anaachiwa kutokana na changamoto za mashahidi" amesema Muhula.

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka shirika la WoteSawa, Joseph Mukoji amesema utoaji wa taarifa kuhusu vitendo vya mmomonyoko wa maadili katika jamii ni muhimu kwa wanajamii.

"Kama ukatili unafanyika katika jamii lazima uripotiwe, bahati mbaya siku hizi tumekuwa na jamii ambayo inaweza kushuhudia vitendo vinavyofanyika kinyume na Sheria na Taratibu za nchi na wasiripoti na kuona kama ukatili huo hauwahusu" amesema Mukoji.

"Sisi walimu tumekuwa tukikemea vitendo viovu na kuhakikisha Sheria na Taratibu za Shule zinazingatiwa hatua inayosaidia kuimarisha maadili katika jamii" amesema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtoni, Mwl. Titi Mwendwa.
Katibu wa Jumuiya ya wazazi Kata ya Mabatini, Haji Said akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Katibu Elimu, Malezi na Mazingira Jumuiya ya Wazazi Kata ya Mabatini, Magabe Mahelesi akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha Polisi Wilaya ya Nyamagana, Kagemlo Muhula akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Afisa Ustawi kutoka shirika la WoteSawa, Renalda Mambo akizungumza na wanafunzi wakati wa maadhimisho hayo.
Mwanasheria kutoka shirika la WoteSawa, Joseph Mukoji akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtoni jijini Mwanza wakiwa kwenye maadhimisho hayo.

No comments:

Powered by Blogger.