Chanzo za wazazi kuwapeleka shule watoto kwa kutumia bodaboa
Na Abby Nkungu, Singida
ELIMU duni katika jamii juu ya Sheria za usalama
barabarani na umasikini wa kipato
vimetajwa kuwa miongoni mwa
sababu za baadhi ya wazazi na walezi kuwasafirisha watoto wao wa chini ya miaka
8 kwa kutumia pikipiki maarufu kama "bodaboda" wakati wa kwenda shule
na kurudi nyumbani, jambo ambalo ni hatari kiafya na linahatarisha usalama na
ulinzi wa kundi hilo muhimu.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama
Barabarani cha Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, Nestory Ndidi wakati
akizungumzia mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Programu Jumuishi ya
Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iliyoanza Januari 2021/2022.
Alisema kuwa licha ya Programu hiyo inayoendelea
hadi 2025/2026 kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kutatua changamoto za Malezi, Makuzi na
Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM); ikiwemo ulinzi na usalama wao, suala la
wanafunzi wadogo kupakiwa kwenye pikipiki limeachwa zaidi kusimamiwa na kikosi
cha usalama barabarani licha ya kuwa ni hatari na linagusa wadau wengi.
“Naam, sisi ndio Wasimamizi wa Sheria za usalama
barabarani ambapo inakatazwa kumpakia kwenye pikipiki mtoto aliye chini ya
miaka 9, ili kulinda usalama na afya yake na hii ni kwa mujibu wa Sheria ya
Wakala wa kudhibiti Usafirishaji wa Ardhini (LATRA) iliyoanzishwa 2010 na
kuanza kufanya kazi rasmi 2011 ambapo vyombo hivyo vya usafiri vilivyoingia kwa
wingi nchini na kuanza kusafirisha abiria” alisema Ndidi
Alifafanua kuwa kutokana na wingi wa bodaboda
karibu kila sehemu nchini, LATRA nao wamekasimisha madaraka hayo kwa
halmashauri za Miji, Majiji na Manispaa ili kusaidia usimamizi wake, lakini kwa
kiasi kikubwa suala hilo limeachwa kwa
Jeshi la Polisi kitengo cha usalama
barabarani.
Hata hivyo, alisema kuwa katika kusimamia sheria
hiyo wanalazimika kutumia busara zaidi kutokana na ukweli kwamba kila
wanapotaka kumsimamisha dereva wa bodaboda naye huongeza mwendo; hivyo kuacha
kuendelea kumfukuza; hasa anapokuwa amepakia mtoto au watoto kwani anaweza
kupata ajali kwa mwendo kasi na kusababisha hatari zaidi kwa afya, ulinzi na
usalama wa mtoto.
Alisema kuwa kupitia utekelezaji wa Programu
Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ipo haja
kwa wadau wote; wakiwemo wazazi, walezi,
walimu na mamlaka zingine kuunganisha nguvu ili kukomesha suala la watoto wa
chini ya miaka 8 kupakiwa kwenye
pikipiki jambo ambalo sio tu ni kinyume cha sheria bali pia ni hatari kwa afya
ya mtoto.
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Singida, Dk.
Hamisi Yuna alisema kuwa kiafya mtoto anayebebwa kwenye pikipiki bila kuwa na
nguo nzito za kumsitiri baridi na upepo njiani anaweza kupata magonjwa ya njia
ya hewa ambayo tiba yake inaweza kugharimu fedha nyingi.
"Taarifa ya magonjwa yanayowakumba watu wenye umri wa miaka 5 na
kuendelea katika Manispaa yetu kwa Januari hadi Machi mwaka huu, inaonesha
magonjwa ya njia ya hewa ndio yanayoongoza kutokana na jumla ya watu 8,572;
wakiwemo watoto wa miaka 5 kuathirika, hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 22"
alifafanua na kuongeza;
"Hivyo, natoa wito kwa wazazi na walezi
kuangalia uwezekano wa kuanza kutumia usafiri mwingine mbadala; kama vile bajaj kwa watoto wa chini
ya miaka minane ili kulinda afya na
usalama wao".
Baadhi ya wazazi na walezi wanasema elimu duni
kwa jamii juu ya Sheria za usalama barabarani na umasikini wa kipato ndio
sababu za kutumia bodaboda kupeleka watoto shule na kuwarudisha nyumbani.
“Mimi nilikuwa sijui kabisaaa kuwa sheria inazuia bodaboda kubabe watoto ndio kwanza nasikia hapa kwako, lakini pia angalieni na kipato basi wazazi wengine hawawezi kumudu gharama za mabasi ya shule maana hiyo tu buku ya kwenda na buku nyingine ya kurudi nyumbani yaani 2000/- kwa siku zinatutoa jasho hali ni ngumu” alisema Shabani Ali mmoja wa wazazi mkazi wa Minga Singida mjini.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Neema Daniel mkazi
wa Mtipa ambaye anasema ingawa baadhi ya wazazi wanatambua hatari licha ya
sheria lakini tatizo ni uwezo wa kifedha ndio maana wanaamua kutumia pikipiki
huku wakimuomba Mungu apishe mbali mabaya yote.
“Watoto wanaamka asubuhi sana kuna wakati
anapakiwa kwenye pikipiki huku akiwa bado na usingizi, ni hatari akilala bado
anapigwa na upepo ambao pia ni mbaya kwa afya yake, lakini hakuna namna zaidi
ya kuomba Mungu tu. Kikubwa, mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu
ya madhara ya kiafya na kiusalama yanayoweza kumkumba mtoto anayetumia pikipiki
kila mara" alieleza.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na viashiria kama vile utapiamlo, umasikini na kukosekana kwa uhakika wa chakula.
No comments: