LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la KIVULINI lashiriki maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI la jijini Mwanza limeshiriki maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Familia Duniani ambayo yameadhimishwa ngazi ya Mkoa Mwanza katika Wilaya ya Ilemela.

Akizungumza Jumatatu Mei 15, 2023 kwenye maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Yassin Ally amesema ni wajibu wa kila mmoja katika jamii kuanzia ngazi ya familia, viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji kuhakikisha suala la maadili linazingatiwa.

Amesema kumekuwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii kutokana na wazazi na walezi kutozingatia malezi bora kwa watoto wao kwani wamejikita zaidi na masuala ya kiuchumi kuliko kufuatilia familia.

Ally amehoji ugumu uliopo kwa wazazi, walezi na viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya jamii kuchukua hatua za kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kama ambavyo wanafanya katika matukio mengine ikiwemo ya kukomesha udokozi mitaani.

Pia ameshauri hatua za kisheria kuchukuliwa kwa baadhi ya nyumba za starehe katika mitaa mbalimbali ya jiji la Mwanza ambazo zimetajwa kuwa vituo vya ukiukwaji wa maadili katika jamii kwa kuruhusu biashara haramu ya ngono kwa wanawake na wanaume kufanyika katika nyumba hizo ambazo pia zinajihusisha na uuzaji wa vilevi vilivyopigwa marufuku kisheria.

Akifungua kongamano la familia wakati wa maadhimisho hayo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Joackim Otaru amesema familia ndiyo taasisi ya kwanza inayomwandaa mtoto kukua katika maadili mema katika jamii hivyo wazazi na walevi ni vyema wakatimiza wajibu huo ipasavyo.

Amesema watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, ulawiti na mimba za utotoni baada ya kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi akisema kwa mwaka 2022 mkoani Mwanza kulikuwa na matukio 255 ya ukatili kwa watoto yaliyoripotwa polisi na hivyo kuwahimiza wazazi kutatua changamoto zinapoibuka ili kutotengana na kuacha watoto wakikosa malezi bora.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Modest Apolinary amesema maadhimisho hayo yamelenga kuwakumbusha wanafamilia kuungana pamoja, kupendana na kuwalea watoto katika maadili ili kuepuka mmonyonyoko wa maadili kama msisitizo uvyowekwa kwenye kaulimbiu ya mwaka huu isemavyo "Imarisha Upendo na Maadili Imara".
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akiwasilisha mada kuhusu ukatili wa kijinsia wakati wa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani yaliyofanyika ngazi ya Mkoa Mwanza katika Wilaya ya Ilemela.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Joackim Otaru akifungua kongamano la maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani yaliyofanyika wilayani Ilemela.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Joackim Otaru akifungua kongamano. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Ilemela, Apolinary Modest na kushoto ni Mstahiki Meya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga.
Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Ilemela, Apolinary Modest akizungumza kwenye kongamano la maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani.
Washiriki mbalimbali wakifuatilia maadhimisho hayo.
Washiriki mbalimbali wakiwa kwenye kongamano la maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani yaliyofanyika ngazi ya Mkoa Mwanza katika Wilaya ya Ilemela, Jumatatu Mei 15, 2023.

No comments:

Powered by Blogger.