LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la WOTESAWA lawaokoa wafanyakazi 165 wakitumikishwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com 
Shirika la kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani WOTESAWA limewaokoa wafanyakazi 165 waliokuwa wakitumikishwa kazi za nyumbani katika kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka huu 2023.

Hayo yamebainika wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Mfanyakazi wa Nyumbani yaliyofanyika Juni 16, 2023 yakiambatana na Siku ya Mtoto wa Afrika.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Meneja wa Nyumba Salama wa Shirika la WoteSawa, Jacqueline Ngalo alisema Shirika hilo limefanikiwa kuwaokoa wafanyakazi hao wa nyumbani na kuwapa huduma mbalimbali ikiwemo mavazi, malazi, chakula, msaada wa kisaikolojia, matibabu pamoja na msaada wa kisheria.

Alisema wafanyakazi 86 tayari wameunganishwa na familia zao huku akitoa rai kwa jamii kuchukua hatua kuwalinda wafanyakazi wa nyumbani kwani wanakumbana na changamoto mbalimbali akisema kwa idadi hiyo ni wazi kwamba kuna changamoto ya utumikishaji wafanyakazi wa nyumbani.

Ngalo alisema miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo wafanyakazi wa nyumbani ni pamoja na kuajiriwa katika umri mdogo, kutokulipwa mshahara stahiki na kwa wakati, kufanyakazi bila kuwa mikataba ya maandishi, kutopewa haki ya likizo na mapumziko mengine yakiwemo ya uzazi huku pia baadhi yao wakikumbana na ukatili na unyanyasi wa kijinsia.

Alitoa rai kwa Serikali kuridhia mkataba wa kimataifa wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani Na.189/2011 hatua itakayosaidia kulinda stahiki za wafanyakazi wa nyumbani huku pia akiomba utekelezaji wa Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini ya mwaka 2004 pamoja na Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 138/1974 unaozuia watoto chini ya miaka 14 kuajiriwa.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa nyumbani, Neema Ishengoma alimuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuridhia mkataba wa kimataifa wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani Na.189/2011 kwani utawalinda wafanyakazi wa nyumbani huku pia aliwasihi kuwapenda, kutowabagua na kuwatimizia stahiki zao kwa mujibu wa mkataba.

Naye Afisa Kazi Mkoa wa Mwanza, Betty Mtega alisema ni kosa kisheria kuwaajiri watoto chini ya umri wa miaka 14 kufanya kazi za nyumbani kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kwenda shule.

Mtega alisema tamko la Serikali kuhusu kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa nyumbani liko wazi na ni vyema waajiri wakalizingatia ambapo mfanyakazi anayeishi kwa mwajiri ni Tsh. 60, 000, wasioishi kwa mwajiri Tsh. 120,000, wanaofanya kazi wa viongozi mashuhuli wakiwemo wabunge Tsh. 200,000 na Tsh. 250,000 kwa wanaofanya kazi kwa wafanyabiashara wakubwa ama viongozi wa kidiplomasia wakiwemo mabalozi.

Maadhimisho hayo yameambatana na kaulimbiu isemayo “Hakuna Usawa wa Kijamii Bila kuwa na Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Nyumbani, Tunaomba Serikali Iridhie Mkataba wa Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Nyumbani, Wakati ni Sasa”.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Afisa Kazi Mkoa Mwanza, Betty Mtega akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Washiriki wakifuatilia maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Mfanyakazi wa Nyumbani pamoja na Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika jijini Mwanza yakiandaliwa na Shirika la WOTESAWA.
Mmoja wa wafanyakazi wa Nyumbani jijini Mwanza akizungumza kwa niaba ya wenzake wakati wa maadhimisho hayo.
Katika maadhimisho hayo, shirika la WOTESAWA liliwatunuku waandishi wa habari saba kutoka vyombo mbalimbali vya habari akiwemo George Binagi kutoka BMG ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao wa kuandika habari kuhusu wafanyakazi wa nyumbani.
Baadhi ya wafanyakazi wa nyumbani jijini Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi meza kuu.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.