LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Misungwi atoa siku 14 mzee wa miaka 95 apate haki yake

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha (kulia) akiwa nyumbani kwa mzee Deus Malosha Nyanda mwenye umri wa miaka 95 (kulia).
***

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Paulo Chacha ametoa muda wa siku 14 kwa kampuni ya Ardhi Plan, kuhakikisha kuhakikisha inatatua mgogoro baina yake na wananchi wa Kijiji cha Bujingwa Kata ya Fella iliowapimia viwanja.

Katika mgogoro huo, Kaya tatu ikiwemo ya mzee Deus Nyanda (95) zinadai kuingia mkataba wa kupimiwa mashamba yao kwa makubaliano ya wao kuchukua asilimia 65 na kampuni kuchukua asilimia 35 lakini baada ya upimaji kufanyika hawakupewa viwanja katika mashamba yao badala yake wakapewa katika mashamba ya wananchi wengine hatua iliyoibua mgogoro wa umiliki.

“Baada ya upimaji kufanyika, shamba langu lilitoa viwanja 50 wakasema watanipa viwanja 32 na kampuni kuchukua viwanja 18, ajabu wakanipa viwanja 10 kwenye mashamba ya watu wengine na hapo ndo ukawa mwanzo wa mgogoro” amesema mzee Nyanda.

Kufuatia malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya Misungwi amefika katika eneo la mgogoro na kuagiza kampuni iliyopima mashamba hayo kwa usimamizi wa ofisi ya ardhi Halmashauri ya Misungwi kukaa na wananchi hao ili kutatua mgogoro huo ndani ya siku 14 kuanzia leo Juni 06, 2023.

“Ofisi yangu ilipokea malalamiko ya mzee Nyanda kwamba asilimia alizopewa siyo walizokubaliana na kampuni ya Ardhi Plan, na hata viwanja alivyopewa haviko kwenye mashamba yake” amesema Chacha na kuongeza;

“Pia waliahidi kumjengea nyumba lakini imejengwa kwa kiwango ambacho hawakukubaliana. Tumeielekeza kampuni hii ya Ardhi Plan kwa kushirikiana na Afisa Ardhi wa Halmashauri imalize huu mgogoro ndani ya siku 14 vinginevyo tutaangalia hatua zaidi za kuchukua” amesema DC Chacha.

Katika hatua nyingine DC Chacha amepiga marufuku kampuni binafsi kupima mashamba ya wananchi bila usimamizi wa ofisi ya ardhi ya halmashauri ya Misungwi huku pia akisitisha uuzaji wa viwanja ikiwemo milima ya mawe inayouzwa kiholela na viongozi wa Serikali za Vitongoji na Vijiji na kuagiza viongozi wa Kijiji cha Idetyemya kurejeshwa shilingi milioni 32 walizouza mlima wa kijiji hicho akisema ametengua makubaliano hayo.

Mwakilishi wa kampuni ya Ardhi Plan, Moses Mtemi amesema kampuni hiyo itafanyia kazi maagizo yaliyotolewa ili kutatua mgogoro huo na kuruhusu shughuli za maendeleo kuendelea katika eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha (kushoto) akizungumza na mzee Daud Nyanda (kulia) mkazi wa Kijiji cha Bujingwa Kata ya Fella ambaye anailalamikia kampuni ya upimaji viwanja ya Ardhi Plan kwa kupima mashamba yake kisha kutompa viwanja stahiki kwa mujibu wa makubaliano.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha (kushoto) akizungumza na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Bujingwa ambao wanadai viwanja vyao vimekabidhiwa kwa mzee Deus Nyanda bila wao kushirikishwa baada ya zoezi la upimaji.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha (wa pili kulia) akizungumza na viongozi wa kampuni ya Ardhi Plan alipofika katika Kijiji cha Bujingwa kusikiliza mgogoro wa viwanja baina ya kampuni hiyo na wananchi kwa ajili ya kuutafutia ufumbuzi.
Afisa Mipango Miji kutoka kampuni ya Ardhi Plan, Joseph Mtemi (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha (kulia) alipofika katika eneo la viwanja vyenye mgogoro baina ya kampuni hiyo na wananchi.
Mwonekano wa eneo lenye mgogo baina ya kampuni ya upimaji viwanja ya Ardhi Plani na wakazi wa Kijiji cha Bujingwa akiwemo mzee Deus Nyanda (95) na wenzake wawili ambao ni Agness George pamoja na Costantine Kupelwa.
Tazama BMG TV hapa chini
SOMA PIA>>> Habari zaidi hapa

No comments:

Powered by Blogger.