LIVE STREAM ADS

Header Ads

Chongolo kujibu hoja za mkataba wa bandari

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo akiwa katika moja ya mikutano yake.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo kesho Julai 23, 2023 anatarajia kuwasha moto katika mkutano wa hadhara ataoufanya Uwanja wa Bombadia mjini hapa ambapo atawahutubia maelfu ya wananchi wa Mikoa ya Singida, Tabora na Dodoma.

Katika mkutano huo ambao ataambatana na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho, ajenda kubwa itakuwa kuhusu mkataba wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam dhidi ya Kampuni ya Dubai Port World (DP World)

Chongolo na viongozi wenzake wanatoa ufafanuzi kuhusu mkataba huo kwa wananchi wa mikoa mbalimbali baada ya kuwepo na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na baadhi ya watu wanaodai kuwa Serikali ya CCM imeingia katika mkataba huo ambao hautakuwa na manufaa kwa nchi.

Chongolo na timu yake tayari amekwishafanya mikutano katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kaskazini, Mikoa ya Kusini na sasa ni zamu ya mikoa ya Kanda ya Kati.

Mikutano yake yote alioifanya katika mikoa hiyo, Chongolo amekuwa akisisitiza kuwa suala la uboreshaji wa bandari sio jambo geni bali lipo katika ilani ya uchaguzi wa CCM ya 2020-2025 chini ya Serikali inayoongozwa na chama hicho.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu akizungumza na waandishi wa habari jana alisema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika kwa asilimia 100 ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Singida kufika kwenye viwanja hivyo kuanzia saa 2:30 asubuhi kwenda kuwasikiliza viongozi hao wa chama hicho kitaifa.

“Maandalizi yote ya mkutano wetu yapo tayari nitumie fursa hii kuwaalika wananchi wote kufika kwenye mkutano huu mkubwa ambao utaambatana na burudani za aina mbalimbali kutoka kwa wasanii wa hapa Singida na nje” alisema Kaburu.

No comments:

Powered by Blogger.