Mbunge Sima awapongeza wananchi kwa ujenzi wa Sekondari
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima akiangalia choo cha Walimu wa Shule ya Msingi Ititi ambacho kimefungwa na kusababisha walimu kukosa sehemu ya kujisaidia alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo aliyoifanya Julai 21, 2023 Kata ya Uhamaka na kujionea changamoto hiyo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima amewashukuru wananchi wa Kata ya Uhamaka kwa usimamizi na ukamilishaji wa ujenzi wa shule bora ya Sekondari jambo ambalo limemuheshima pamoja na Rais Samia Suluhu Hassam ambaye alitoa zaidi ya Sh.Milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Sima alitoa shukurani hizo Julai 21, 2023 alipokuwa akihutubia kwenye mkutano wa hadhara baada ya kutembelea na kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi za kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
"Tulikuwa na changamoto kubwa mbili za shule na umeme nilimuomba Mungu siku nikija kusimama tena katika viwanja hivi ziwe zimetekelezeka hama zinatekelezeka na leo ninapo simama hapa shule tayari imekamilika na wanafunzi wanasoma na ninyi ni mashahidi kwa jinsi kulivyokuwa na changamoto kubwa ya elimu vijana walivyokuwa wakitembea zaidi ya kilometa 17 kwenda Shule ya Sekondari ya Mandewa ambayo ilikuwa na wanafunzi wengi kuliko uwezo wake" alisema Sima.
Alisema kufuatia changamoto hiyo alijenga hoja kwa kuomba shule mbili lakini aliambiwa atapewa fedha za shule moja hivyo aeleze zipelekwe wapi ambapo hakufikiria na kueleza zipelekwe kwenye kata hiyo ya Uhamaka.
"Niwashuru sana sehemu nyingine kumekuwa na changamoto kubwa ya ukamilishaji wa miradi ya Serikali fedha zinapelekwa lakini haikamiliki ninyi hapa Uhamaka mmekuwa tofauti mmeshiriki vizuri na kuhakikisha shule yenu imekuwa ya kiwango bora na ya mfano ambapo kila viongozi wamekuwa wakifika kuitembelea jambo ambalo najivunia mno" alisema Sima.
Wakati huohuo Sima aliwaomba wananchi wa Mtaa wa Ititi kuanza mara moja ujenzi wa vyoo vya Shule ya Msingi kwa ajili ya wanafunzi na walimu kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo walimu hawana kabisa choo huku wanafunzi wakijisaidia kwa kusubiriana kutokana na kuwepo kwa choo kimoja tu.
Kwa wakazi wa Uhamaka aliwaambia waanze ujenzi wa Kituo cha Afya baada ya Zahanati inayotumika sasa majengo yake kuchakaa na kuwa na nyufa nyingi na kuelemewa kutokana na idadi kubwa ya watu ambao wanakwenda kupata huduma na kuwa ilijengwa miaka ya 1950 wakati watu wakiwa wachache.
"Nawaombeni anzeni ujenziwa maeneo haya mawili ili nikajenge hoja tuweze kuongezewa nguvu ya ujenzi kwani Serikali yetu ambayo ni sikivu chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassani tunaweza kupatiwa fedha za kukamilisha ujenzi huo lakini kikubwa ni lazima na ninyi kuonesha mmeanza kufanya kazi hiyo kwa umoja na nguvu zenu" alisema Sima.
Akizungumzia suala la umeme alisema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Desemba 29, 2022 ilizindua mradi mpya wa kusambaza umeme kwenye Vijiji Miji viliyopo pembezoni mwa Manispaa ya Singida ambao utagharimu Sh. 7.11 Bilioni na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ndilo msimamizi wa mradi huo.
Alisema Kata ya Uhamaka ni moja ya mnufaika wa mradi huo wa kusambaza umeme katika Vijiji Miji (Peri-urban Electrification) na kuwaeleza wananchi hao wauchangamkie kwa kuanza kusuka nyaya za umeme katika nyumba zao ili waweze kufungiwa kwa gharama ya Sh.27,000.
"Mradi huu ukikamilika unakwenda kubadilisha uchumi wa wanananchi kwani watautumia umeme huo kuanzisha viwanda vidogo na shughuli zingine za uzalishaji ambazo zitatumia nishati hiyo hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla" alisema Sima.
Alisema hivi sasa tayari katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo nguzo zimekwishwa simikwa na kuwa mradi huo utaanza kufanya kazi wakati wowote.
Mbunge Sima akizungumzia kuhusu mkataba wa Bandari ya Dar es Salaam dhidi ya Kampuni ya DP World ya Dubai aliwata wananchi wa kata hiyo kuwapuuza wale wote wanaotaka kupotosha ukweli wa mkataba huo wenye tija kwa nchi yetu kuwa eti Rais Samia Suluhu Hassan ameiuza bandari hiyo.
Alisema wabunge wasingeweza kuridhia kufanyika kwa maridhiano ya mkataba huo baina ya Tanzania na DP World iwapo kama kungekuwepo kwa viashiria vya kuuzwa kwa bandari hiyo.
Alisema kupitia uwekezaji huo Tanzania itakuwa ikipata Sh.Trilioni 26 kwa mwaka tofauti na sasa ambapo tunapata Sh.Trilioni 7 tu kupitia bandari hiyo kwa mujibu wa taarifa zilizopo.
Alisema hata hivyo suala hilo litazungumzwa kwa kirefu na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo katika mkutano wa hadhara utakofanyika leo Viwanja vya Bombadia ambapo ataambatana na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho na wananchi watapata uelewa kuhusu jambo hilo.
Katika ziara hiyo Mbunge Sima alitembelea Shule ya Msingi ya Ititi na kujionea changamoto kubwa ya kutokuwa na vyoo ambapo pia alitembelea Shule ya Msingi ya Uhamaka na kuona baadhi ya madarasa yakiwa na nyufa jambo ambalo linahatarisha maisha ya wanafunzi.
Eneo lingine ambalo alitembelea ni Zahanati ya kata hiyo ambayo pia alikuta majengo yake yakiwa na nyufa huku mbao za paa lake zikiwa zimeoza,ambapo pia atembelea Shule Mpya ya Sekondari ya Uhamaka na alipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi na kuwataka kuzingatia masomo na kufuata maadili yatakayo wafanya watimize ndoto za maisha yao.
Diwani wa Kata hiyo Senge M. Senge alipata fursa ya kuelezea miradi iliyokamilika na thamani yake na changamoto kadhaa zilizopo ikiwa ni pamoja na barabara ya kutoka katika kata hiyo na kuunganisha na barabara kuu ya kutoka Igunga kwenda Dodoma eneo la Ititi Manispaa ya Singida.
Mbunge Sima, akihutubia wananchi wa Kata ya Uhamaka baada ya kutembelea na kukagua baadhi ya miradi.
No comments: