LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wasanii watakiwa kuchangamkia mabilioni ya Rais Samia

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga akizungumza wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo mkoani humo jana.

Na Dotto Mwaibale, Lindi
Wasanii mkoani Lindi wametakiwa kuchangamkia fedha Sh.Bilioni 20 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kama ruzuku za kuwawezesha kukopa ili kuwasaidia kuinua vipato vyao kupitia kazi zao za sanaa.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

"Hizi fedha zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili yenu hivyo changamkieni fursa hiyo kwa kuboreha shughuli zenu ili muweze kujikwamua kiuchumi" alisema Ndemanga.

Alisema wadau wa Sanaa watakaokidhi vigezo vilivyoweka ndio watakaokopeshwa fedha hizo kupitia mfuko ulioanzishwa na Rais Samia ambapo aliwahimiza wasanii hao kuhakikisha wanakithi vigezo hivyo ili waweze kukopesheka na kuwa fedha hizo sio zawadi bali zinatakiwa kurejeshwa ili ziweze kukopeshwa kwa wengine.

Shahibu aliwataka wasanii hao na wadau wa utamaduni kujiendeleza kielimu ili kwenda na dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia huku wakianzisha miradi mbalimbali kama ufugaji,kilimo, na mingine badala ya kutegemea sanaa peke yake.

Aidha, aliwataka wasanii hao kujenga tabia ya kushirikiana na taasisi zingine wakati wa kufanya shughuli zao jambo ambalo litawaongezea uzoefu wa masuala mengine ya maendele na sanaa kwa ujumla.

Alisema Serikali inatambua mchango wa wasanii na kuwa kwa siku za hivi karibuni imeonekana kazi nyingi za wasanii kama filamu na tamthilia zikioneshwa zaidi na vyombo vya habari vya watu binafsi hivyo watawasiliana na wahusika wa vyombo vya Serikali kuona namna ya kuanza kutumia kazi za wasanii hasa chipukizi katika vyombo hivyo.

"Changamoto kubwa iliyopo ni uzingatiaji wa maadili katika kazi zetu nawaombeni mkawe mabalozi wazuri wa kusimamia maadili ya kitanzania na si vinginevyo na kuacha kutengana kwa sababu ya migogoro yakugombea fedha na sisi kama Serikali hatutakuwa tayari kuona mambo hayo yakitokea" alisema Ndemanga.

Awali akitoa taarifa ya mfuko huo Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tazania Nyakaho Mahemba alisema mfuko huo unatoa huduma katika maeneo ya urithi wa utamaduni , lugha na fasihi, sanaa za maonyesho, ufundi , filamu, muziki na fani nyingine zenye mlengo wa utamaduni na sanaa kwa watu binafsi, vikundi au makundi.

Alitaja huduma zinazotolewa na mfuko huo kuwa ni mikopo ya uendeshaji yenye lengo la kuwezesha shughuli za kiutendaji wa kila siku za uzalishaji wa kazi za utamaduni au sanaa.

Alitaja kazi nyingine ni utoaji wa mikopo ya vifaa yenye lengo la kuwezesha ununuzi wa vitendea kazi vya uzalishaji za utamaduni au sanaa na mikopo ya kujikimu/ dharura ambayo ni mikopo ya muda mfupi inayotolewa kwa lengo la kujikimu wakati wa safari za kuandaa au kufanikisha kazi za utamaduni au sanaa.

Alisema lengo la mafunzo ni kuongeza ujuzi na thamani ya kazi za utamaduni na sanaa ili ziwe na ubora unaoendana na mahitaji ya soko.

Mahemba alisema kulingana na kuingia makubaliano na Benki ya CRDB na Serikali kupitia mfuko huo walengwa wa mfuko watakaohitaji huduma za mikopo watatakiwa kuwasilisha maombi yao kwa njia ya posta, barua pepe au moja kwa moja katika ofisi za mfuko huo kwa ajili ya mapitio ya awali ya kitaalamu kisha maombi hayo kufikishwa katika Benki ya CRDB kwa hatua zao.

Msanii wa ngoma za asili Salum Namtitili akizungumza kwa niaba ya wenzake alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fedha hizo kwa lengo la kuwainua kiuchumi.

“Tunaishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wasanii kwani tulikuwa na changamoto kubwa ya kuendeleza sanaa zetu lakini kwa fedha hizi tutasonga mbele kwani tutaweza kutoka sehemo moja kwenda nyingine na kurekodi kazi zetu tofauti na ilivyokuwa zamani tukiangaika kutafuta fedha huku na kule bila ya mafanikio” alisema Namtitili.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga (katikati) akiwasili Hoteli ya Sea View Hotel and Resort kwa ajili ya kufungua warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tazania Nyakaho Mahemba akitoa taarifa ya mfuko huo.
Afisa Utamaduni Mkoa wa Lindi, Makalaghe Nkinda, akizungumza kwenye warsha hiyo.
Afisa Mwandamizi wa Mkopo wa Benki ya CRDB kutoka Makao Makuu, Alpha Mgubila, akizungumza kuhusu mikopo itakayokopeshwa kwa wasanii kupitia benki hiyo.
Mwenyekiti wa Wasanii Mkoa wa Lindi, Athuman Mohamed akizungumza kwenye warsha hiyo.
Msanii wa ngoma za asili, Salum Namtitili, akitoa shukurani kwa Rais Samia kwa kutoa fedha hizo.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa warsha hiyo.
Wasanii wakiwa kwenye warsha hiyo.
Viongozi wakiimba wimbo wa kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo.
Wasanii wakiimba wimbo wa kumshukuru Rais Samia.Wasanii wakiwa kwenye warsha hiyo.
Warsha ikiendelea.
Wasanii wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi.

No comments:

Powered by Blogger.