LIVE STREAM ADS

Header Ads

Maadhimisho ya Nanenane Mwanza yanoga, RC Mwanza atoa maagizo kwa Maafisa Ugani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amewataka maafisa ugani wa Kanda ya Ziwa Magharibi kuwatembelea wakulima na wafugaji ili kuwakumbusha juu ya kuzingatia kanuni bora za Kilimo na ufugaji ili kuweza kupata tija kubwa kwenye Uzalishaji.

Makalla ametoa rai hiyo Agosti 08, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Kanda ya Ziwa Magharibi katika Kilele cha Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yaliyowakutanisha kwa Siku 8 Mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza ambapo ameyafunga rasmi.

"Wataalamu msichoke kuwatembelea wakulima na wafugaji na kuwapa ushauri stahiki na katika maeneo yenu ya kazi anzisheni mashamba darasa ili wakulima waendelee kujifunza na kuyaona mafanikio" amesisitiza Makalla.

Ametoa wito kwa vijana kuacha kufanya kilimo mtandaoni na uvuvi haramu badala yake amewataka kujikita kwenye kilimo na ufugaji wa kisasa wa samaki kwani Rais Samia amekua akitoa fedha nyingi kwenye kuwainua vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ya aina mbalimbali.

"Tafiti mbalimbali juu ya zao la pamba zinaonesha kwenye ekari moja mkulima anaweza kupata kilo 800 had 1200 wakati hali halisi ya mavuno kwa mkulima ni kati ya kilo 150 hadi 300 na kwa ng'ombe wa maziwa anaweza kufikia lita 25-30 kwa siku wakati hali halisi kwa sasa lita 10 kwa ng'ombe" Makalla.

Makalla amebainisha kuwa Mkoa wa Mwanza katika msimu wa 2022/23 ulilima hekta 455,498.05 na kuzalisha tani 634,373.78 sawa na asilimia 80 hadi kufikia Juni na akabainisha kuwa elimu waliyoipata hapo itawasaidia kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Emily Kasagara amefafanua kuwa maonesho hayo yamewapa fursa wadau kutoka sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ambazo huhusisha utafiti, umwagiliaji pamoja na hifadhi za Mazao kujifunza kwa vitendo.

"Katika Maonesho ya Kilimo na sherehe za Wakulima (Nane nane) 2023 jumla ya wadau 863 waneshiriki. Idadi hii inajumuisha Mamlaka za Serikali za Mitaa13, Taasisi za Serikali 11, Tltaasisi za fedha 07, taasisi za elimu 10, makampuni ya zana za kilimo 09 pamoja na wajasiriamali wakubwa na wadogo 746" amesema Kasagara.

Maadhimisho hayo ya 2023 yameenda sambamba na kaulimbiu: "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula."

No comments:

Powered by Blogger.