LIVE STREAM ADS

Header Ads

Maonesho ya Nane Nane 2023 Ngongo mkoani Lindi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele Programu ya Korosho,Kitengo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Wadudu waharibifu na Magonjwa, Bobnoel Assenga (kushoto) akitoa maelezo ya Wadudu waharibifu na Magonjwa kwa mkulima Cathbert Richard (kulia) aliyetembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya NaneNane 2023 yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi. Katikati ni Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano wa taasisi hiyo.


Dotto Mwaibale na Godwin Myovela, Lindi
KITUO cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele kilichopo mkoani Mtwara kimekuwa kivutio kikubwa katika Maonesho ya Nanenane 2023 Kanda ya Kusini yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Katika Maonesho hayo kituo hicho kinatarajia kuonesha teknolojia za kilimo za kuvutia wakulima kutoka Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi ambao wameombwa kujitokeza kwa wingi kufika katika viwanja hivyo kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo hicho Dk. Fortunus Kapinga kuhusu maonesho hayo Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mawasiliano alisema wamejipanga vizuri na kuwa wakulima wategemee kupata ujuzi mkubwa wa masuala ya kilimo katika maonesho hayo.

Alisema TARI Naliendele ni miongoni mwa vituo 17 vilivyopo chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania ambapo pia wanavituo vingine kama hivyo katika kanda zingine nchini na kueleza kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha teknolojia zinawafikia wakulima.

Alisema TARI Naliendele wamepewa jukumu la kitaifa la kutafiti zao la korosho, ufuta na karanga na kuwa changamoto zote zinazojitokeza kwenye mazao hayo wao ndio wanaowajibika kutoa majibu.

Kidunda alisema pia wamekuwa wakifanya utafiti wa mazao mengine kwa kushirikiana na vituo vingine vilivyopewa mamlaka kitaifa na kuwa katika maonesho hayo wana programu ya utafiti wa mazao ya nafaka, mikunde, jamii ya mizizi, mbogamboga na matunda.

Alisema mwaka huu wamejipanga vilivyo kuonesha teknolojia zote za kilimo na litakuwa ni tukio la aina yake kwani kwa wale waliozoea kufika kwenye siku za nanenane sasa wataona shughuli endelevu za kituo hicho na kuwa wamefanya maboresho lukuki ya kisayansi katika kila idara.

" Kituo cha Ngongo sio kwa ajili ya Nanenane tu bali kipo kwa mwaka mzima kueneza teknolojia za kilimo na wataweza kuangalia teknolojia mbalimbali za korosho, mbegu za mafuta, mikungu ya ndizi ya aina Mtwike , jamii ya mikunde na nafaka. Mbali ya hayo pia kutakuwa na shughuli ya kuangalia jinsi ya kuongeza thamani ya zao la korosho, ufuta na zao la karanga ambapo katika zao la korosho watu walizoea kuja na kutafuna korosho lakini sasa watakuja kula na kunywa korosho kwani watakuwa na juisi, jamu na mvinyo zilizotokana na zao hilo" alisema Kidunda.

Alisema katika maonesho hayo watakuwa na kituo chao cha kanda ambacho kitatumika kutoa mafunzo kwa wakulima hivyo wadau mbalimbali wameombwa wafike kwani wataona mengi kwenye zao la korosho, ufuta, karanga, mihogo, viazi vitamu, kunde, choroko, mbaazi, mahindi, uwele na mengineyo.

Alisema mazao yote ambayo yanalimwa kwenye mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi na hata yale ambayo hayalimwi katika mikoa hiyo lakini yanaweza kustawi maeneo hayo yatakuwepo katika maonesho hayo.

Kidunda alisema katika kituo chao cha Naliendele wamekuwa hawana msimu pale wameweka teknolojia ambazo zinaonekana kwa mwaka mzima kwa ajili ya wakulima kujifunza hatua mbalimbali za ukuaji wa zao husika kuanzia likiwa kwenye kitalu, shambani, utumiaji wa viatilifu, udhibiti wa magonjwa na uvunaji wake.

" Tukisema mkulima au mdau aje wakati wa wiki ya Nanenane tu kuna hatua nyingi hawezi kuzielewa na ndio maana tunasema hatufungi maonesho haya tupo kipindi chote cha mwaka mzima." alisema Kidunda.

Alisema TARI imekuwa ikisogeza huduma zake kwa wananchi nchi nzima ili ziwafikie walengwa.

Alisema zamani zao la korosho lilikuwa likilimwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani lakini sasa linalimwa karibu mikoa zaidi ya 20 kama Morogoro, Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Katavi, Mbeya, Rukwa, Iringa, Njombe, Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya Same.

Alisema kinachosemwa korosho ilimwe wapi sio mipaka ya kiutawala bali ni mahitaji ya kiikolojia.

Kidunda alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima na wadau mbalimbali kufika kwenye maonesho hayo ya Kanda ya Kusini yanayofanyika Ngongo mkoani Lindi kuanzia Agosti 1,2023 kwenda kujifunza teknolojia za kilimo ambayo yatafikia tamati Agosti 8, 2023.

Kidunda alisema akiwa kama Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano jukumu lake kubwa ni kuhakikisha teknolojia zinawafikia wakulima.

"TARI Naliendele tunafanya utafiti na ukishafanywa kazi yetu ni kutoa matokeo ya utafiti huo na idara yangu kazi yake kubwa ni kuuchambua na kuchakata taarifa za utafiti huo na kuziweka katika lugha nyepesi ambayo inaweza kuwa rahisi kwa wakulima na wadau wengine kuielewa" alisema Kidunda.

Kidunda alisema kauli mbiu ya maonesho hayo mwaka huu ni Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula.

Mtafiti kutoka TARI Naliendele Programu ya Korosho, Kitengo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Wadudu waharibifu na Magonjwa, Bobnoel Assenga alisema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wakulima namna ya kudhibiti visumbufu vya wadudu waharibifu na magonjwa, ikiwemo ugonjwa wa Ubwiriunga, ugonjwa wa Blaiti na Debeki ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni changamoto kwa ustawi wa zao la korosho ndani ya Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na kwingineko
nchini.

Alisema Tari Naliendele imekuwa ikikabiliana na kukithiri kwa wadudu waharibifu wa zao hilo wakiwemo Mbu wa Mikorosho, Mbu wa Minazi na Vidung’ata ambao ni kikwazo kikubwa cha ukuaji mzuri wa zao la Korosho ambalo linatajwa kuwa ni zao lenye uchumi mkubwa na soko la uhakika.

Assenga alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima kufika katika banda la TARI kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo.
Maelezo yakitolewa kwa wakulima waliotembelea banda la TARI.
Afisa Kilimi Msadizi wa TARI Naliendele, Justina Misungwi, akiwapa watoto juisi iliyotengenezwa kwa zao la korosho walipotembelea banda la taasisi hiyo.
Wakulima Ahmadi Mnenele (kushoto) na Mathayo Milanzi (kulia) wakiangalia ndizi aina ya Mtwike ambayo imetokana na utafiti uliofanywa na TARI na kuleta tija. Katika ni Mtafiti wa Kilimo kutoka TARI, Zamira Matumbo.
Muonekano wa Jengo la TARI katika Maonesho hayo.
Afisa Kilimo Msaidizi, Noel Mwigune (kulia) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi, Jitulize ambao walitembelea kuona mazao ya nafaka yaliyofanyiwa utafiti na TARI.
Muonekano wa shamba la mbogamboga katika maonesho hayo.
Mtafiti Msaidizi wa Kilimo kutoka TARI, Dickson Malulu (kulia) akitoa maelezo ya kilimo cha kebichi kwa wakulima Calvin Michael (kushoto) na Evarist Eprahim waliotembelea shamba hilo
Mtafiti wa zao la ufuta kutoka TARI, Mohamed Fadhil, akitoa maelekezo lwa wakulima kutoka Wilaya ya Nachingwea kuhusu kilimo cha zao hilo.
Muonekano wa zao la ufuta aina ya Ziada katika maonesho hayo.
Muonekano wa zao la Muhogo aina ya Kiloba katika maonesho hayo.

No comments:

Powered by Blogger.