LIVE STREAM ADS

Header Ads

MSD yaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mhandisi wa vifaa tiba wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kati Dodoma, Jumanne Mapesa (kulia) akimkabidhi boksi la dawa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Paul Ndeki mjini Singida Oktoba 11, 2023. Wengine ni wafanyakazi wa hospitali hiyo.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) imetoa vifaa tiba na dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 532.4 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Hospitali ya Wilaya ya Singida, Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Hosptali ya Wilaya ya Ikungi na Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu mkoani hapa.

Akizungumza Oktoba 11, 2023 wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwenye hospitali hizo, Meneja wa MSD Kanda ya kati Dodoma, Bi. Mwanashehe Jumaa amevitaja vifaa tiba na dawa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kuwa ni vitanda 9 (ICU Beds) vya kisasa pamoja na dawa..

Amesema kwa Hospitali ya Wilaya ya Singida vifaa vilivyotolewa ni vitanda viwili wakati kwa Kituo cha Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ni pasi ya kunyoshea nguo, vitanda vya wagonjwa, vitanda vya kujifungulia, mashuka, magodoro na viti mwendo..

Jumaa amesema utoaji wa vifaa hivyo ni muendelezo wa uboreshaji wa huduma za sekta ya afya mkoani Singida kwani Machi 15, 2023 MSD ilitoa mashine za kufulia, vifaa vya kinywa na meno, usingizi na vitanda Hosptali ya Wilaya ya Singida Ilongero.

Baada ya kukabidhi vifaa hivyo, wataalam kutoka MSD walitoa maelekezo kwa wataalam ambao hospitali zao zimenufaika na vifaa hivyo wavitunze ili vidumu muda mrefu kwani Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua.

"Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kununua vifaa hivi hivyo ni wajibu wa watumishi wa sekta ya afya kuhakikisha vinatunzwa vizuri" amesema Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna.

Viongozi wa Hospitali hizo wameishukuru serikali kupitia MSD kwa kuendelea kuwapatia dawa na vifaa tiba kwa wakati jambo ambalo limeongeza tija na ufanisi wa kazi katika utoaji huduma za afya

Nao Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Paul Ndeki, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Singida, Yusuph Kitinya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itigi, Emmanuel Mallange, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hussein Sapoko waliahidi kuvitunza na kumshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.

“Vifaa tulivyopatiwa vitatusaidia kutoa huduma zetu tunawashukuru Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa vifaa tiba kupitia MSD hivyo kuhimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi” amesema Kitinya.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli amesema wamepokea vitanda 16 na kufikisha idadi ya vitanda 80 na kueleza kuwa mbali ya vifaa hivyo pia walipokea baadhi ya vifaa vingine vingi kama magodoro, mashuka, taa za kufanyia uchunguzi, taa ya chumba cha upasuaji na sasa wapo kwenye mchakato wa kupelekewa mashine itakayosaidia kufanya operesheni ya mama na mtoto katika jengo ambalo lipo mbioni kukamilika.

"Kwa ujumla ni idadi kubwa ya vifaa tulivyoletewa na Serikali chini ya mama yetu kipenzi Rais Samia kupitia MSD" amesema Dkt. Kimotoli.

Kwa upande wake Mganga wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Hussein Sepoko amesema Rais Samia amewapelekea vifaa tiba vingi vya kisasa na akaishukuru MSD kwa ushirikiano inayowapa wa kuwapelekea vifaa tiba na dawa kwa wakati.

Nao Diwani wa Kata ya Ilongero Issa Mwiru na Diwani wa Kata ya Itigi Mjini, Ally Minja walipongeza Serikali na MSD kwa kusambaza vifaa tiba na dawa.

“Kwa nafasi ya kipekee tunaishukuru MSD wamekuwa na ushirikiano mkubwa tunapohitaji vifaa tiba na dawa wanatuletea kwa wakati hakika wameendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya" amesema Mwiru.

Aidha, Mwiru ameishukuru Serikali kwa kuwaletea watumishi katika hospitali mpya ya Wilaya ya Singida na kusifia utendaji kazi wao kwa masaa yote wanapokuwa kazini.

MSD imemaliza kufanya kazi ya kusambaza vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba Kiomboi na Ikungi hata hivyo wataendelea kufanya hivyo kulingana na mahitaji ya vifaa tiba na dawa mkoani Singida. .
Makabidhiano ya vitanda (ICU Bed) na magodoro yakifanyika Hosptali ya Rufaa Mkoa wa Singida.
Moja ya kitanda kati ya tisa vilivyotolewa na MSD vikishushwa kwenye gari.
Vitanda vikishushwa.
Wafanyakazi wa Sekta ya Afya wa Hospitali ya Wilaya ya Singida wakionesha furaha yao wakati wakipokea vitanda viwili (ICU Bed) kutoka MSD.
Mwonekano wa mashine ya kukaushia nguo iliyopelekwa na MSD Katika Hospitali ya Wilaya ya Singida.
Mashine ya kufulia nguo iliyotolewa na MSD ukiwa Hospitali ya Wilaya ya Singida.
Mapokezi ya vitanda (ICU Bed) yakifanyika Hospitali ya Wilaya ya Singida. Katikati ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Singida, Yusuph Kitinyi.
Diwani wa Kata ya Ilongero, Issa Mwiru (mwenye fulana rangi ya njano( akiwa na viongozi wengine baada ya kupokea vitanda hivyo.
Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna (wa pili kulia) akimkabidhi vifaa tiba Diwani wa Kata ya Itigi Mjini, Ally Minja na viongozi wengine.
Gari la MSD likishusha vifaa tiba Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida.
Mhandisi wa vifaa tiba wa MSD Kanda ya Kati Dodoma, Jumanne Mapesa (wa pili kushoto) akipeana mkono na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli baada ya kumkabidhi vitanda 25 vya kawaida vya wagonjwa Oktoba 12, 2023.
Vitanda vya kawaida vya wagonjwa vikishushwa kutoka kwenye gari la MSD tayari kwa makabidhiano wilayani Ikungi.
Muonekano wa moja ya kitanda cha kawaida cha wagonjwa kati ya vitanda 80 vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD vilivyopo Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.
Mhandisi wa vifaa tiba wa MSD Kanda ya Kati Dodoma, Jumanne Mapesa (kushoto) akishiriki kubeba vifaa tiba wakati wa makabidhiano wilayani Iramba.
Mhandisi wa vifaa tiba wa MSD Kanda ya Kati Dodoma, Jumanne Mapesa akipeana mkono na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hussein Sepoko baada ya kumkabidhi vitanda viwili (ICU Bed) vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD.
Dereva wa MSD, Kanda ya Kati Dodoma, Mrisho Gyumi (kushoto( akiwajibika kubeba moja ya boksi la vifaa tiba kabla ya makabidhiano wilayani Iramba.

No comments:

Powered by Blogger.