LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Makilagi ahimiza matumizi sahihi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi 2022

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi akifungua mafunzo ya matumizi sahihi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo ya matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.


Mkuu wa Wilaya ya Nyamaga mkoani Mwanza, Amina Makilagi amesema matumizi bora ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yataongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kazi sanjari na kusaidia kurahisisha upatikanaji wa maendeleo katika Wilaya hiyo.

Ameyasema hayo Jumatano Oktoba 11, 2023 wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi, watendaji, wenyeviti wa mitaa pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.

Mafunzo hayo ya siku moja ambayo yameandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu yamefanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza.

Makilagi amesema Matokeo ya Sensa ni msingi wa maendeleo ya Taifa kwa kuwezesha upangaji wa mipango ya maendeleo, Sera na Programu zenye kuleta maendeleo kwa haraka kwa kuzingatia mahitaji ya jamii.

"Sisi Wilaya ya Nyamaga bajeti yetu ya mwaka huu tumeiandaa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa na tunaamini kuwa itasaidia kuharakisha shughuli za maendeleo hususani kwenye maeneo ambayo yanauhitaji wa huduma mbalimbali za kijamii" amesema Makilagi.

Aidha Makilagi amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia elimu waliyoipata kwenye mipango yao ya kazi hatua itakayosaidia kufikisha huduma za kijamii ikiwemo umeme, maji na masoko kwa wakati.

Meneja Idara ya Shughuli za Takwimu, Benedict Mugambi amesema Serikali ipo katika utekelezaji wa awamu ya tatu na ya mwisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ambapo kazi zinazofanyika ni pamoja na uchakataji, uchambuzi, uandishi wa ripoti na usambazaji wa matumizi ya matokeo ya Sensa.

"Miongoni mwa ripoti ambazo ziko katika hatua ya mwisho kukamilika ni ripoti ya taarifa za msingi za kijamii, kiuchumi na kidemografia, ripoti ya majengo kwa aina na mgawanyo wake kwa maeneo ya utawala ambapo ripoti hizi zitazinduliwa rasmi kabla ya Disemba 2023" amesema Mugambi akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukru Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuwapa mafunzo ambayo yatawasidia kutekeleza kwa weledi majukumu ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Meneja Idara ya shughuli za Takwimu, Benedict Mugambi akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi, watendaji, wenyeviti wa mitaa na wawakilishi wa makundi ya kijamii jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.