LIVE STREAM ADS

Header Ads

Rais Samia anatamani mradi wa JNHPP uanze kazi- Dkt. Biteko

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona mradi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaanza kufanya kazi ili watanzania wapate umeme wa uhakika.

Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo Oktoba 24, 2023 jijini Dar es salaam alipokutana na kufanya kikao na ujumbe wa Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi kutoka nchini Misri, Dkt. Assem Elgazzar kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa JNHPP.

Dkt. Biteko amesema Rais Samia ana mategemeo makubwa kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo na anatamani mwanzoni mwa mwaka 2024 utekelezaji wake uanze na kuongeza kuwa mradi wa JNHPP ndio mwarobaini wa kutatua changamoto ya hali ya upatikanaji wa umeme nchini.

Ameishukuru Serikali ya Misri kwa kuonyesha ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo kwa wakati na kusisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Elgazzar ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiamini nchi hiyo katika kutekeleza mradi huo. Pia amesema mradi huo utakua wa mfano katika ufuaji wa umeme.

Naye Balozi wa Misri nchini Tanzania, Sherif Ismail ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo wa Bwawa la kufua umeme la JNHPP.
Mradi wa bwawa la kufua umeme la JNHPP unatekelezwa na kampuni ya Arab Contractor kutoka nchini Misri na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 92.74 ambapo majaribio ya mradi huo yanatarajiwa kufanyika Januari 2024.

Kikao hicho pica kimehudhuriwa na ujumbe wa TANESCO, kampuni inayotekeleza mradi wa JNHPP (Elsewedy Electric na Arab Contractors) ya nchini Misri na wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati.

No comments:

Powered by Blogger.