LIVE STREAM ADS

Header Ads

RC Simiyu ataka miradi ya umeme kukamilika kwa wakati

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme ya msongo wa KV 220 Shinyanga (Ibadakuli) hadi Simiyu (Bariadi), pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Simiyu kukamilisha mradi huo haraka ili wananchi waondokane na adha ya umeme.

Dkt. Nawanda ametoa maagizo hayo 25 Oktoba 2023 katika ziara yake katika Wilaya ya Maswa na Bariadi iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi huo.

"Tunataka ndani ya miezi 18 kipindi cha Mkataba mradi uwe umekamilika na utekelezaji wa mradi usiwe na mashaka mashaka na wamenihakilishia hapa kuwa kazi hii itakamilika ndani ya muda uliopangwa" amesema Dkt. Nawanda.

Aidha Dkt Nawanda ameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufikisha umeme katika Vijiji 470 ndani ya Mkoa wa Simiyu.

"Vijiji vya Mkoa wa Simiyu hatumdai umeme Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kazi tuliyo nayo ni kusafirisha umeme katika Vitongoji baada ya mradi huu wa kusafirisha umeme KV 220 kukamilika" amesema Dkt. Nawanda.

Kwa upande wake meneja wa mradi huo, Mhandisi Adolf Kigombola amesema tayari kazi za awali zimeanza kutekelezwa na mkandarasi baada ya TANESCO kwa kushirikiana na wadau wa mradi kufanya uhamasishaji kwa wananchi ili kuruhusu uanzaji wa kazi za awali wakati Serikali ikichakata malipo ya Fidia.

Ameongeza kuwa TANESCO inafuatilia kwa karibu malipo ya fidia kwa waathirika wa mradi na kwamba wananchi watarajie malipo ya fidia mapema mwezi Novemba 2023.

Mkandarasi M/S Kalpataru Projects International Limited (KPIL) kutoka nchini India anatekeleza ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme ya msongo wa KV 220 Shinyanga (Ibadakuli) hadi Simiyu (Bariadi), huku kituo cha kupoozea umeme ujenzi wake ukitekelezwa na M/S Sian Electric Engineering Co.LTD kutoka nchini China.

Serikali imeelekeza kiasi cha shingi Bilioni 48 kwa ajili ya Utekelezaji wa mradi huo ulioanza utekelezaji wake 10 Machi 2023 ambapo unatarajiwa kukamika ifikapo 9 Septemba 2024.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu

No comments:

Powered by Blogger.