LIVE STREAM ADS

Header Ads

Dawati la kushughulikia ukatili wa kijinsia lazinduliwa TIA Singida

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Dawati la Jinsia wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, Mkaguzi wa Polisi Amina Abdallah, ambaye alikuwa mgeni rasmi akizungumza na Wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakati akizindua rasmi dawati la jinsia Oktoba 01, 2023.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limezindua rasmi dawati la jinsia katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa taasisi hiyo.

Mkuu wa Dawati la Jinsia wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, Mkaguzi wa Polisi Amina Abdallah akizungumza Novemba 01, 2023 kwenye uzinduzi huo, amesema dawati hilo litasaidia kwa wanafunzi wanaopatwa na madhira kutoa taarifa ili changamoto zao ziweze kufanyiwa kazi.

Amesema viongozi wa dawati hilo ambao watakuwa wanapokea taarifa kabla ya kuzifikisha ngazi za juu wazingatie suala la usiri ili wanafunzi waweze kuwa na imani na dawati hilo.

Abdallah amepongeza uongozi wa taasisi hiyo kwa kazi nzuri ambayo imesaidia kudhibiti vitendo vya unyanyasa wa kijinsia katika msimu wa masomo uliopita hakujaripotiwa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia yakiwamo ya ubakaji na ulawiti ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

"Huu utaratibu wa kuwa na dawati la kijinsia usiishie katika taasisi hii bali uenezwe katika vyuo vingine na shule za msingi kwa kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na hiyo ndio itakuwa njia nzuri ya kukabiliana na matukio hayo" amesema Abdallah.

Katika kuhakikisha dawati hilo linapata nguvu kushughulikia changamoto za unyanyasaji wa kijnsia kwa wanafunzi, walichaguliwa wajumbe watatu kulisimamia ambao ni Waziri wa Afya kutoka Serikali ya Wanafunzi ya taasisi hiyo, Ramla Mchomvu, Mkutubi Francis Majele na Mlezi wa wanafunzi, Asia Hansy.

Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Flora Lemnge amewataka wanafunzi hao watakapokuwa na changamoto yoyote ya ukatili wa kijinsia kwenda kutoa taarifa kwa wajumbe hao ambao ni wasiri na wanauzoefu mkubwa ambapo kwa wavulana aliwataka kwenda kumuona Mkutubi Francis Majele.

Mshauri wa wanafunzi katika taasisi hiyo, Ambwene Kajula amesema wanafuraha kulizindua dawati hilo licha ya kuwa nalo na kuwa lengo la kulizindua ni kutaka kuukataa na kuutokomeza kabisa ukatili katika jamii yao na watu wawe bora kama Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alivyoamua kuweka Wizara ya Ustawi wa Jamii na kuona kazi ya dawati la jinsia lina msaada mkubwa.

"Dawati la jinsia linasaidia kuweka mazingira bora kwa wanafunzi na kama wataweza kuongea na kupata sehemu ya kusema madhira yao walioyapata kwa ukaribu tena kwa mtu ambaye amemzoea ni jambo jema sana" amesema Kajula.

Amesema katika kampasi hiyo wamechaguliwa baadhi ya walimu na watumishi kuwa wajumbe wa dawati hilo ambao watasaidia kupokea taarifa kutoka kwa waathirika na kuzifanyia kazi na kuyafikia malengo ya kutokomeza ukatili katika taasisi hiyo na nchi kwa ujumla.

Mwanafunzi wa taasisi hiyo anayesomea ngazi ya cheti, Pendo Maube akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema kupitia uzinduzi huo wameweza kujua fursa mbalimbali ambazo zinapatikana katika dawati hilo la kijinsia kama kujua haki zao na namna ya utoaji wa taarifa pale panapotokea changamoto ya ukatili wa kijinsia.

Katika uzinduzi huo elimu mbalimbali imetolewa ambapo Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida , Mwantumu Bakari akiongozana na wataalamu wa jeshi hilo walitoa mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto ambapo walitoa namba ya kutoa taarifa iwapo kutatokea changamoto hiyo kwa kupiga namba 114.

Aidha viongozi mbalimbali wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) mkoani hapa nao wamepata fursa ya kutoa elimu ya kupinga vitendo vyote vya ukatili na walitoa namba 116 ya kupiga kwa ajili ya kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ambapo wanafunzi hao walikubali kuwa mashujaa wa Smaujata.

Mbali ya elimu hiyo kutolewa na makundi hayo pia baadhi ya wawakilishi wa taasisi za kifedha kama benki ya NMB, CRDB na nyingine nao walitoa elimu ya namna ya utunzaji wa fedha ambapo walielezea umuhimu kwa wanafunzi hao wa kufungua akaunti ili kutunza fedha zao badala ya kuwa nazo kwenye mabegi na kukosa usalama.
Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Mratibu wa Taaluma, Flora Lemnge akizungumza katika uzinduzi huo.
Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida, Mwantumu Bakari akitoa elimu ya jinsi ya kukabiliana na majanga ya moto.
Mshauri wa Wanafunzi katika taasisi hiyo, Ambwene Kajula, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Naibu Smaujata Mkoa wa Singida, Kabelwa Ramadhani akizungumza na wanafunzi wa TIA Kampasi ya Singida.
Afisa Kumbukumbu na Nyaraka wa TIA Singida, Juma Kihiyo akizungumzia jinsi mwanafunzi anavyotakiwa kuomba ruhusa ya kutoka chuoni.
Katibu Gavana wa Wilaya ya Singida, Miraji Hamisi akizungumza.
Katibu Idara ya Wanawake Smaujata Mkoa wa Singida, Evelyne Lyimo akichangia jambo kwenye uzinduzi huo.
Makamu Mwenyekiti Idara ya Wanawake Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Hapiness Francis akichangia jambo wakati akitoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na mambo mengine.
Mwenyekiti wa Smaujata Manispaa ya Singida, Elineema Babu, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Elimu ya kukabiliana na majanga ya moto ikitolewa na Afisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Wanafunzi wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi ukiendelea.
Wanafunzi wakishiriki uzinduzi huo.
Saluti ikipigwa wakati wimbo wa taifa ukiimbwa.
Mwenyekiti Idara ya Vijana Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Manispaa ya Singida, Omari Mwangi, akitoa nasaha zake kwa wanafunzi wa kampasi hiyo.
Shujaa mtoto wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii ambaye hakupenda kutaja jina lake naye alikuwepo kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi huo ukiendelea.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi
Mgeni rasmi wa uzinduzi huo, Mkaguzi wa Polisi, Amina Abdallah (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa dawati la jinsia Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.Kutoka kushoto ni Ambwene Kajula, Ramla Mchomvu, Asia Hansy na Francis Masele.
Muonekano wa moja ya gari la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambalo linatumika kuzima moto.

No comments:

Powered by Blogger.