LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wabunge wavutiwa na Skimu ya umwagiliaji Mkalama

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ujenzi wa mradi wa skimu ya umwagiliaji uliopo Kijiji cha Msingi Kata ya Msingi wilayani Mkalama mkoani Singida Novemba, 14, 2023..


Na Dotto Mwaibale, Singida
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa skimu ya umwagiliaji uliopo Kijiji cha Msingi Kata ya Msingi wilayani Mkalama mkoani Singida ambao serikali imetoa zaidi ya Sh. Bilioni 34.

Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo wilayani Mkalama Mwenyekiti wa kamati Daniel Sillo ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Raymond Mndolwa kwa kazi kubwa inayoifanya ya kukamilisha miradi hiyo ya ujenzi wa mabwawa ambayo ni muhimu kwa Taifa ukiwemo mradi huo wa Skimu ya Umwagiliaji Kata ya Msingi Mkalama.

Sillo amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na kuwa mradi huo na mingine yote itakapo kamilika inakwenda kuchangia ongezeko la fedha katika bajeti ya Serikali.

Sillo amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anataka kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji kwa wananchi kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Aidha, Sillo amewataka wananchi wasijenge kwenye eneo la mradi hasa kwenye mashamba yanayotarajia kulimwa kwani mradi huu ukikamilika utawanufaisha wao kwa kulima zaidi ya mara moja kila mwaka .

Sillo ameiomba Wizara ya Kilimo hasa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kusimamia vizuri mradi huo na kukamilika kwa wakati ili uwe na tija kwa wananchi na Taifa.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde amempongeza Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji . Raymond Mndolwa kwa kusimamia vizuri ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

Silinde amesema serikaki inataka wananchi walime si kwa kutegemea mvua na kwamba mradi huo utakapokamilika utaongeza pato la mwananchi sababu atakuwa anavuna zaidi ya mara mbili kwa mwaka na pia itaongeza pato kwa halmashauri na usalama wa chakula nchini.

Akizungumzia suala la wananchi kuanza kujenga katika mashamba, Silinde amesema ni kwasababu wanafahamu nini kinakwenda kutokea na kuwataka waache serikali itengeneze miundombinu ya mradi huu kwani lengo la serikali ni kuondokana kwenye kilimo cha kienyeji kuja kwenye kilimo cha kisasa chenye tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa amesema ujenzi wa mradi huo utakapokamilika unatarajia kuwanufaisha zaidi ya wakazi 12,000 wa vijiji vinne vilivyopo Kata ya Msingi.

Aidha ameieleza kamati hiyo kuwa wananchi wameanza kujenga nyumba kwenye eneo la mradi huo hivyo kuanza kupoteza eneo la kilimo ambapo aliomba eneo la uwekezaji thamani yake ni vema likabaki lile lile vinginevyo manufaa ya uwekezaji itakuwa ni bure.

Mndolwa amewaomba viongozi wa serikali ya wilaya na mkoa iingilie kati suala hili kwa kuwazuia wananchi wasiendelee kujenga mashambani kwani Sh.Bilioni 34 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya mradi huu ni fedha nyingi.

Hata hivyo, Mndolwa amesema tume itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa na kuwa miradi yote inayojengwa itakamilika kwa wakati na serikali inaendelea kutoa fedha kwa aajili ya utekelezaji.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu, Mhandisi Fuko Koyoya amesems mradi huu ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 utawanufaisha wakazi 12,000 wa vijiji vinne vya Ishinsi, Ndurumo, Msingi na Kidi vilivyopo Kata ya Msingi tarafa ya Kinyangiri ambao watalima mazao ya mpunga,mahindi na mbogamboga Kwa misimu miwili hadi mitatu kwa mwaka.

Amesema shughuli zitakazofanyika katika mradi huu ni ujenzi wa bwawa lenye ujazo wa Lita 1,875,000, ujenzi a mifereji ya umwagiliaji yenye kilometa 19.12, uchimbaji wa mifereji ya matupio yenye urefu wa kilo mita 42.539, uchimbaji wa mifereji ya kuingiza Maji mashamba yenye urefu wa jumla ya kilometa 34.778.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara za mashamba zenye urefu wa kilomita 36.1, kusawazisha ekari 2,000 za mashamba,ujenzi wa kilomita nane za barabara na makaravati sita kuelekea ndani ya mradi na ujenzi wa vigawa Maji 14,vipunguza mwendo, viumbo angalizi 90, vipitisha maji 90, makaravati 14 pamoja na vivuko nane.
Mradi huo ambao umeanza kujengwa Julai Mosi mwaka huu unatarajia kukamilika Disemba 14, 2024.
Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa akisisitiza jambo mbele ya kamati hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu, Mhandisi Fuko Koyoya akitoa taarifa ya mradi huo.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde akizungumza wakati wa ziara hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Daniel Sillo akizungumzia mradi huo.
Mjumbe wa kamati hiyo, Zaituni Swai akijitambulisha.
Mjumbe wa kamati hiyo, Rashid Abdalla Rashid akijitambulisha.
Mjumbe wa kamati hiyo, Reuben Kwagilwa akijitambusha.
Mjumbe wa kamati hiyo, Shally Raymond akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, Francis Isack akishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo ambao ni muhimu kwa wananchi na taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali (kulia) akizungumza wakati akiwakaribisha wajumbe wa kamati hiyo.
Wajumbe wa kamati hiyo wakiwa kwenye ziara hiyo wilayani Mkalama.
Wajumbe wa kamati hiyo wakiwa kwenye ziara hiyo wilayani Mkalama.
Safari kuelekea ulipo mradi huo ikifanyika.
Mwonekanao wa ujenzi wa skimu hiyo ya umwagiliaji.

No comments:

Powered by Blogger.