LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanawake wang'ara mahafali ya 21 Taasisi ya Uhasibu Singida

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda (katikati) akiongoza maandamano ya wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakati wakiwasili kwenye mahafali ya 21 ya taasisi hiyo yaliyofanyika Novemba 17, 2023. Kulia kwake ni Wakili Said Chuguma ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Sherehe za Mahafali ya 21 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida imemalizika huku idadi kubwa ya wanawake ikizidi kuongezeka mara dufu ikilinganishwa na idadi ya wanaume.

Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo jumla ya wanawake 938 sawa na asilimia 55.2 wamehitimu katika mahafali hayo Kampasi ya Singida ikilinganishwa na idadi ya wanaume 762 sawa na asilimia 44.8.

Akizungumza kwenye mahafali hayo yaliyofanyika Novemba 17, 2023 Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo amesema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 1,700 katika kampasi hiyo kati yao wanawake 938 sawa na asilimia 55.2 na wanaume 762 sawa na asilimia 44.8, wamepata tunuku zao kwenye fani mbalimbali.

Amrsema jumla ya Wahitimu ngazi ya Cheti cha Awali ni 567, Astashahada 452, Stashahada 491, na Shahada 190.

Profesa Pallangyo amesema idadi hiyo kubwa ya wahitimu wanawake inadhihirisha kwamba TIA inanaunga mkono jitihada za Serikali, kwa kutoa fursa ya mafunzo pasipo ubaguzi.

Amesema idadi ya wahitimu wote wa TIA kwa mwaka wa masomo 2022/2023 kwa Kampasi za Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Singida ni 13,218 ambapo wanawake ni 7,139 sawa na asilimia 54 na wanaume ni 6,079 sawa na asilimia 46.

Amesema wanaposherehekea mahafali hayo ya Ishirini na moja TIA imepiga hatua kubwa katika uendeshaji wa mafunzo, huduma ya ushauri wa kitaalam, rasilimali watu, pamoja na miundombinu ya kusomea na kufundishia katika kampasi hii ya Singida.

Amesema idadi ya wanachuo wanaodahiliwa katika Kampasi ya Singida imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Mathalani, katika mwaka huu wa masomo 2023/2024, ulioanza Mwezi Oktoba, 2023, jumla ya wanachuo 1,443 wamedahiliwa katika kampasi ya Singida.

Ameongeza kuwa hata hivyo, zoezi la usajili bado linaendelea na lengo ni kudahili wanachuo wapya 2,600 ukilinganisha na udahili wa wanachuo 1,556 katika mwaka wa masomo 2022/2023.

Amesema ongezeko hilo la wanafunzi kwa kiasi kikubwa linatokana na mambo makubwa matatu ambayo ni ubora wa elimu itolewayo inayotokana na mitaala inayowajengea wanachuo wa ngazi zote msingi wa umahiri hivyo kumwezesha mhitimu kuajiriwa na hata kujiajiri pindi anapohitimu masomo yake. Hatua hii huwafanya wazazi na wanafunzi kuichagua TIA.

Utaratibu mzuri wa Serikali wa kuwapangia vyuo moja kwa moja wahitimu wa kidato cha nne waliofaulu na kukidhi vigezo (kupitia TAMISEMI). Mathalan, katika mwaka wa masomo 2023/2024 jumla ya wanafunzi 1,170.

"Ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada hatua ambayo imewezesha watanzania wengi wenye sifa kumudu gharama za masomo. Kwa mfano, katika mwaka huu 2023/2024 Serikali imepanga kuwafadhili wanachuo 810 wa shahada katika kampasi hii ya Singida na hili ni ongezeko la asilimia 15.9 ukilinganisha na wanachuo 699 waliofadhiliwa mwaka 2022/2023" amesema Pallangyo.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo alisema amefurahishwa sana na mpango wa ukuzaji na uendelezaji wa wanafunzi kitaaluma na kitaalamu yaani (Career Development Program) wanaoufanya kwa wanafunzi wa taasisi hiyo kwa kujitengenezea fursa muhimu za kibiashara kwa kuendeleza ubunifu wao ambao ni fursa adhimu kwa wanafunzi hao.

“Mmedhihirisha umahiri wenu, na kutupa wasaa wa kushuhudia matunda ya juhudi zenu. Hivyo, sina budi kwa niaba ya Serikali, kutoa pongezi zangu za dhati kwa Uongozi, Wahadhiri na wafanyakazi Waendeshaji, kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chote cha mafunzo yenu.

Safari yenu ya mafunzo haikuwa nyepesi; safari yenu ilihitaji uvumilivu, ushirikiano, nidhamu, kujituma na zaidi ya yote kumtegemea Mungu. Kwa pamoja, haya ndiyo yamewawezesha kufikia hatua hii muhimu” Mwenda ametoa pongezi hizo kwa niaba ya Serikali.

Aidha, Mwenda aliwaasa wahitimu hao kwamba, hatua waliyoifikia iwe ni chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la ajira na kujiajiri na kuwa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inahimiza sana Taasisi zote kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wanafunzi iwe elimu, ujuzi na maarifa ya kukidhi mahitaji ya soko ili itumike kuleta tija na maendeleo yanayoendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo, akizungumza kwenye mahafali hayo.
Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema akiwatambulisha wageni waalikwa.
Mhitimu wa Shahada ya Uhasibu kutoka kampasi ya Singida, Patrick Edward akipokea cheti kutoka kwa mgeni rasmi.
Viongozi wa TIA wakiwa kwenye mahafali hayo. Kutoka kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa TIA, Dkt. Momole Kasambala, Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha na Utawala TIA, Dkt. Issaya Hassanal na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko TIA, Lilian Rugaitika.
Mratibu wa Taaluma, Flora Lemnge akizungumza.
Viongozi wakiwa meza kuu. Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha, Thabiti Dokodoko, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Wakili Said Chiguma, Mgeni rasmi wa Mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Afisa Mtendaji wa TIA, Profesa, William Pallangyo na Mkurugenzi wa TIA, Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema.
Wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wakiwa kwenye maandamano kuelekea kwenye viwanja vya mahafali hayo.
Wahitimu wa Shahada ya Uhasibu wakionesha furaha yao kabla ya kutunukiwa vyeti vyao.
Viongozi mbalimbali na Waadhiri wa TIA wakiwa wamejipanga foleni tayari kwa kumpokea mgeni rasmi wa mahafali hayo.
Mkuu wa Idara ya Mpango wa ukuzaji na Uendelezaji wa Wanafunzi Kitaaluma na Kitaalamu yaani(Career Development Program) wa taasisi hiyo, Imani Matonya (mwenye suti katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajasiriamali wanafunzi wa TIA Kampasi ya Singida wakati wakimsubiri mgeni rasmi kuona bidhaa zao na kuzungumza nao.
Taswira ya mahafali hayo.
Mratibu wa Ujasiriamali na Kituo Atamizi wa Kampasi ya Singida, Mohamed Kaluse, akizungumza kwenye mahafali hayo ya 21.
Wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wakionesha furaha zao baada ya kutunukiwa vyeti vyao.
Waadhiri wa TIA wakiwa kwenye mahafali hayo.

No comments:

Powered by Blogger.