LIVE STREAM ADS

Header Ads

Zambia yatua Tanzania kujifunza mbinu za kupambana na ujangili

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Timu ya Maafisa Wandamizi kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Zambia vinavyohusika na uzuiaji ujangili wamefika nchini kwa lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika mapambano dhidi ujangili.

Timu hiyo iko nchini kwa siku tano kuanzia Oktoba 29 hadi 4 Novemba 2023.

Akizungumza baada ya kutembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara, Kamishna wa uzuiaji ujangili nchini Zambia, Brigedia Jenerali, Herman Kamwita ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Zambia alisema wamekuja kuona namna Tanzania ilivyofanikiwa kuendesha operesheni za kupambana na ujangili na utekelezaji wa Mkakati wa kupambana na ujangili.

Amesema Kamisheni ya kudumu ya Tanzania na Zambia ya Ulinzi na Usalama ilipendekeza Mamlaka ya nchi hizo mbili kuwa na utaratibu wa kubadilisha uzoefu katika kulinda rasilimali za wanyamapori na misitu.

Amesema wameweza kupitishwa katika mbinu mbalimbali ambazo Tanzania inatumia katika kupambana na ujangili na kuwa wamepanga kwenda kuzitumia wakirudi nchini kwao.

Ameongeza kuwa "pia tumepata fursa ya kwenda Hifadhi ya Ziwa Manyara na tumeona wanyama mbalimbali na hii imedhihirisha namna wenzetu walivyopiga hatua kwenye uhifadhi na niwahakikishie kuwa tutakwenda kutumia mbinu hizi ili kuimarisha sekta ya utalii nchini kwetu.’’

Awali Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uzuiaji Ujangili na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Taifa, Kiza Yusuph Baraga esema wamepokea ugeni kutoka Zambia na kuwa kupitia ziara hiyo pande hizo mbili zimebadilishana uzoefu.

"Pia imekuwa ni nia ya nchi yetu kuendelea kutangaza utalii hasa kutokana na juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza Utalii kupitia filamu ya The Royal Tour "

Amesema ugeni huo pia umepata fursa ya kujionea vivutio vya utalii baada ya kutembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara na kushuhudia shughuli mbalimbali za utalii ambazo zinafanywa kwa teknolojia ya hali ya juu.

"Wamefurahi sana na wametuahidi kuwa sehemu ya kutangaza utalii wetu nchini Zambia. Nitoe wito kwa watalii mbalimbali husani wa ndani ya nchi na nje ya nchi kuja kutembelea vivutio vyenye wanyama wengi".

Naye Kamshina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Betrida Lyimo alishukuru wizara kupeleka ugeni huo katika Ikolojia ya Tarangire Manyara na kuwa wameweza kubadilishana mambo mengi.

Kwa upande wake Wakili Mwandamizi Ofisi ya Mashtaka Makao Makuu ambaye pia ni Mratibu wa upelelezi, uendeshaji wa kesi za makosa ya rushwa, udanganyifu na utakatishaji fedha sehemu ya makosa ya mazingira na maliasili wa Kikosi cha Taifa ya Kupambana na Ujangili Theophil Daniel Mutakyawa alisema kupokea ugeni huo na kubadilisha uzoefu ni mwanzo wa kushirikiana katika kupambana na ujangili kwa kubadilishana taarifa.

Amesema makosa ya ujangili ni makosa yanayovuka mipaka yanayohitaji nguvu ya pamoja ya nje ya nchi, kikanda katika kupambana uhalifu huo mkubwa.

"Tumezungumza na kuelewana kuwa sasa wanaporudi nchini kwao na sisi kubaki huu utakuwa mwanzo wa kuendelea kupeana uzoefu, kupeana taarifa ili tuweze kupambana na uhalifu mkubwa".

No comments:

Powered by Blogger.