LIVE STREAM ADS

Header Ads

Dkt. Biteko ahimiza viongozi kuacha alama katika utumishi wao

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa
wito kwa viongozi mbalimbali Serikalini kuhakikisha kazi
walizonazo wanazifanya kwa bidii kubwa na kuacha alama nzuri kwa
wananchi, hivyo ni muhimu kazi hizo zikaonekana na kufaidisha
wananchi.

Amesema hayo Desemba 05, 2023 akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada maalum ya kuaga mwili wa Baba Askofu Mstaafu, Dkt. Erasto Kweka iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro.

Ibada hiyo maalum imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa na Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.

“Baba Askofu Kweka ameacha alama nzuri duniani kwani ameanzisha vitu vingi ambapo hata kama ameondoka, vitu hivyo vinaendelea kuonekana na kufaidisha wengine, enzi ya uhai wa Baba Askofu alitoa mchango mkubwa katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kuleta usawa wa kijinsia, uanzishwaji wa miradi ya maji safi ndani na nje ya Dayosisi, elimu, Chama cha Akiba na Mikopo na Benki ya Uchumi ya KKKT ambayo inawahudumia watu wote na madhehebu yote” amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii
na kutokuta tamaa, akitolea mfano wa maisha ya Marehemu Baba Askofu
Kweka ambaye alianza kutafuta maisha akiwa kijana mdogo baada ya
kufiwa na Baba yake akiwa na umri wa miaka 14 mpaka hatua aliyofikia
sasa ya mafanikio kwa Kanisa la KKKT na watu wanapata huduma kupitia
juhudi zake.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan anatambua mchango wa Marehemu Baba Askofu Kweka kwenye maendeleo ya Kanisa la KKKT na kwamba Serikali itauenzi mchango wake katika Sekta pia za Afya, Elimu na Maji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania
(KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Onaeli Shoo
amesema viongozi wa Kanisa hilo wamefarijika na uwepo wa viongozi wa Serikali waliojumuika nao kutoka siku msiba ulipotokea mpaka wakati wa Misa hiyo Maalum.

Pia ametoa pole kwa Wananchi na Serikali kufutia maafa yaliyotokea
katika Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara ambapo baadhi ya wananchi
wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa kufuatia maporomoko ya ardhi na ameeleza kuwa Kanisa linafarijika na juhudi mbalimbali
zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika
kutatua changamoto katika eneo hilo, na tayari Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa Majaliwa yupo katika eneo la maafa na timu kutoka kwenye
ofisi yake.

Marehemu Baba Askofu Mstaafu, Dkt. Erasto Kweka alizaliwa Aprili 24, 1934 katika Kijiji cha Mamba Uswaa wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro ambapo enzi ya uhai wake alitumika katika nyanja mbalimbali ikiwemo Ualimu, kabla ya kuingia ngazi ya Utumishi wa
Kanisa.

Mwaka 1973 alichaguliwa kuwa Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya
Kaskazini wadhifa alioutumikia hadi mwaka 1976 ambapo mwaka mmoja
baadaye alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini na pia
kukaimu nafasi ya Mkuu wa Kanisa kabla ya kustaafu kwa heshima mwaka
2004.

No comments:

Powered by Blogger.