LIVE STREAM ADS

Header Ads

Rais Mstaafu Kikwete, Mtenda Mkuu GPE watembelea Shule za Msingi Dar

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Bi. Laura Frigenti, Desemba 1,2023 wametembelea na kukagua shule za Msingi ya Maji Matitu iliyoko Mbagala na Mikongeni iliyoko Gongo la Mboto jijini Dar es salaam.

Ziara hiyo ambayo Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Juma Kipanga na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Deo Ndejembi pia walikuwepo,ambapo imefanyika siku tatu kabla ya mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi wa GPE utakaofanyika Zanzibar kuanzia mapema wiki ijayo.

Madhumuni ya ziara hiyo ilikuwa ni kukagua na kujionea shule ambazo Shirika hilo limetoa ufadhili.

Katika shule ya Maji Matitu shirika hilo limefadhili ujenzi wa madarasa nane na matundu 20 ya vyoo, wakati katika shule ya Mikongeni imechangia ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo.

Akiongea baada ya ziara hiyo, Dkt. Kikwete ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na GPE katika kuboresha sekta ya elimu hasa hasa kwa wasichana na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi na mikakati ya kuiendeleza sekta hiyo.

Dkt. Kikwete ambaye ni Mwafrika wa kwanza kuongoza GPE amesema shirika hilo hadi sasa limeishaipatia Tanzania jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 332 (takriban shilingi 834,980,332,000.00) ili kusaidia sekta ya elimu bara na visiwani.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Frigenti ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kusaidia juhudi za kuendeleza sekta ya Elimu hususani katika nchi zenye uhitaji, akisisitiza kwamba changamoto nyingi za kimaisha zinaweza kuepukika endapo wananchi watapatiwa elimu bora.

Frigenti ameeleza kuridhishwa kwake na matumizi ya Fedha ambayo GPE imekuwa ikitoa kwa Tanzania na kusema kuahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo na uliodumu kwa miaka 10 sasa.

Fringeti ameisifia Serikali kwa kuendelea na juhudi zake za kuendeleza elimu kwa kujenga miundo mbinu bora na kuhakikisha kila mtoto anapatiwa elimu.

Novemba mwaka huu GPE imetiliana saini na Serikali ya makubaliano ya kutoa dola za Kimarekani milioni 85 (takriban shilingi 213, 775, 085, 000.0) kwa ajili ya kusaidia mafunzo ya walimu nchini.

Dkt. Kikwete, akiwa mwenyekiti wa GPE ataongoza vikao vya Bodi vya Shirika hilo huko Zanzibar kuanzia tarehe 4 hadi 6 Disemba, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa Shirika hilo la kimataifa kufanya vikao vyake vya bodi barani Afrika.

GPE iliyoanzishwa mwaka wa 2002, ni Shirika linalosimamiwa na Benki ya Dunia, linalofadhili maendeleo ya elimu ya msingi na utendaji wa sera za nchi zinazoendelea.

Majukumu ya GPE ni pamoja na kusaidia serikali za nchi zinazoendelea kufanya mabadiliko ya kimfumo na kuoanisha rasilimali na ufadhili ili kutoa elimu bora kwa watoto Wote, kuinua viwango vya kujifunza na kukabiliana na changamoto mpya.

Aidha Dkt. Kikwete, akiwa mwenyekiti wa GPE ataongoza vikao vya Bodi vya Shirika hilo huko Zanzibar kuanzia tarehe 4 hadi 6 Disemba, na tayari wajumbe wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali duniani wameanza kuwasili nchini.

No comments:

Powered by Blogger.