LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mahafali ya 26 Chuo Kikuu SAUT, Dkt. Biteko atoa nasaha kwa wahimu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini baada ya kuajiriwa au kujiajiri, wakasikilize na kuhudumia watu wa makundi yote hasa maskini kwani kila mwananchi ana haki ya kupata huduma bora bila kujali hadhi aliyonayo.

Amesema hayo katika Mahafali ya 26 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (SAUT), tarehe 16 Desemba 2023 yaliyofanyika katika viwanja vya Raila Odinga SAUT jijini Mwanza.

"Ndugu Wahitimu na wale ambao tupo makazini, tusikilize watu wa makundi yote hasa wale wasio na kitu cha kutulipa na tuone fahari ya kunyanyua hadhi ya watanzania kwenda kwenye maisha yaliyo bora zaidi kwani ukisaidia maskini unakuwa umesaidia wananchi wengi zaidi" amesema Dkt. Biteko

Aidha Dkt. Biteko ametaka Wahitimu nchini kuchukia rushwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwaeleza kuwa, waone fahari kuchukia rushwa na waichukie kwa kuonekana kwa macho ili kutoa heshima kwa vyuo na nchi kwa ujumla.

Dkt. Biteko amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa kila mtu mwenye juhudi na kuhakikisha kwamba mazingira ya kufanya kazi yanakuwa bora, pia Serikali itaendelea kuweza mazingira mazuri ya uwekezaji, na kuendelea kuajiri kila itakapopata nafasi za kuajiri wahitimu wenye taaluma mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma salam za pongezi kwa jumuiya ya wana SAUT na wahitimu kwa Mahafali hayo ya 26.

Amesema Rais anaamini kwamba, uwepo wa Taasisi hiyo ya SAUT inaongeza mchango mkubwa katika mipango ya Serikali katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi kupitia wahitimu wa kada mbalimbali katika chuo hicho.

Kwa wahitimu wote, Dkt. Biteko amewaasa kwamba watoe huduma kwa haki na waende kujifunza kwa walio makazini kwani kujifunza hakukomi na waendelee kupata ujuzi kupitia ngazi nyingine za masomo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema eneo la chuo cha SAUT litawekwa taa za barabarani ili kuongeza usalama kwa wanafunzi katika chuo hicho akieleza kuwa Mkandarasi wa kufanya kazi hiyo ameshapatikana.

Kuhusu barabara katika eneo hilo ambalo alielezwa na viongozi wa Chuo kuwa si rafiki ameahidi kuwa Serikali nalichukua suala hilo na italifanyia kazi.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha SAUT, Profesa Costa Ricky Mahalu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kuvisimamia na kuviendeleza Vyuo vikuu nchini ambavyo vimeendelea kuzalisha wahitimu wa kada mbalimbali.

Pia ameshukuru uhusiano mzuri ulipo kati ya Serikali na Chuo hicho ambao umepelekea kupata wanafunzi wa kutosha kila mwaka katika kada mbalimbali na mikopo inayotolewa kupitia Bodi ya Mikopo ambayo inawajumuisha wanafunzi ngazi ya astashahada.

Katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 3,066 wamehitimu masomo yao katika ngazi mbalimbali ikiwemo Shahada ya Uzamivu katika Mawasiliano ya Umma, Shahada ya Uzamili ya Utawala na Biashara, Shahada ya Uzamili ya Uchumi na Shahada ya Uzamili ya Sheria.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria Mahafali hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makala, Mhashamu Baba Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga,
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Wengine ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania na
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC); Mhashamu Baba Askofu Flavian Kasala wa Jimbo
Katoliki la Geita, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania na Makamu wa
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Balozi Profesa Costa Ricky Mahalu, Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania.

No comments:

Powered by Blogger.