LIVE STREAM ADS

Header Ads

Rais Samia ataka usimamizi mzuri zana za wavuvi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanawasimamia vyema wavuvi waliokopeshwa boti na vizimba ili wazitumie zana hizo kwa matumizi sahihi yatakayosaidia kupunguza uvuvi haramu nchini 

Rais Samia ameyasema hayo Jumanne Januari 30, 2024 jijini Mwanza wakati akizungumza kwenye hafla ya ugawaji wa vizimba 222 vya kufugia samaki na boti za kisasa 55 kwa wavuvi Kanda ya Ziwa.
Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya walinufaika na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya zana hizo ili kusaidia ukuaji wa sekta ya uvuvi.

Ameeleza kuwa shughuli zote za uvuvi nchini lazima ziendeshwe kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili rasilimali za uvuvi ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijavyo.

"Uvuvi haramu unarudisha nyuma maendeleo ya wavuvi, pia unajenga chuki kati ya wavuvi na Serikali, hivyo niwaombe Wizara ya Mifugo na Uvuvi muongeze kasi katika kusambaza zana hizi za mikopo na kutoa elimu ili wavuvi waondokane na uvuvi haramu " amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema kutokana na uhitaji wa watanzania kuwa na zana za kisasa, wamezamilia kutoa takribani boti 800 nchini zitakazowafaa wavuvi.

Amesema zana zilizotolewa kwa wavuvi zitawawezesha kufikia malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/25, mpango wa tatu wa maendeleo ya miaka mitano 2021 hadi 2025, Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 2015 na mpango kabambe wa uvuvi wa mwaka 2022/23 hadi 2036/37.

Aidha ameeleza kuwa kutokana na maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika katika sekta hiyo yatasaidia kuongeza pato la Taifa kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 10 ambapo pia itaongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi kwa asilimia 35 kutoka kwenye uzalishaji wa sasa ambao ni tani laki tano hadi laki saba kwa mwaka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema utafiti uliofanywa mwaka 2018 hadi 2022 unaonesha samaki katika Ziwa Victoria wamepungua kwa asilimia 30 na kuathiri uendeshaji wa viwanda.

"Tulikuwa na viwanda 15, lakini vinavyofaya kazi ni vinane hadi sasa, tumeathiriwa na uvuvi haramu, Mkoa umeshachukua hatua mbalimbali na kuweka mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu ili tuweze kuwa na uvuvi endelevu" amesema Makalla
 Miongoni mwa wanufaika wa zana za uvuvi zilizokabidhiwa kwa wavuvi Kanda ya Ziwa ni Kilisanti Mtenya ambaye ameiomba Serikali kujenga viwanda vya kuchakata chakula cha samaki katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kurahisisha upatikanaji wa chakula hicho kwa bei nafuu.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.