LIVE STREAM ADS

Header Ads

Rais mstaafu Ally Hassan Mwinyi afariki

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi amefariki dunia Februri 29, 2024 majira ya saa 11 jioni katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Saratani ya mapafu.

Taarifa ya msiba huo imetangazwa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amesema awali Hayati Mzee Mwinyi alikuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba 2023 London nchini Uingereza na baadaye kurejea nchini kuendelea na matibabu katika hospitali ya Mzena.

Kufuatia msiba huo, Rais Samia ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia Machi 01, 2024.

"Kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais mstaafu wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia leo Februari 29 saa 11 jioni katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu" amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema kutokana na msiba huo, bendera zitapepea nusu mlingoti kwa siku saba kuanzia Ijumaa Machi 01, 2024.

"Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa letu. Nchi yetu itakuwa katika kipindi cha siku saba za maombolezo, ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia kesho Machi 01, 2024. Hayati Mzee Ally Hassan Mwinyi atazikwa tarehe 02 Machi 2024 huko Unguja, kisiwani Zanzibar. Inna Lillahi wa inna ilayhi raaji'un" amesema Rais Samia.

Mzee Mwinyi amefariki dunia akiwa na miaka 98, miezi tisa na siku 21. Sawa na siku 36,091.

Mei 08, 1925 ndiyo tarehe ambayo Mwinyi alizaliwa. Kijiji cha Kivure, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Mwinyi akiwa mtoto, alipelekwa Zanzibar kusoma madrasa (elimu ya dini ya Kiislam). Tangu hapo, Mwinyi alikulia na kusoma Zanzibar hadi kufikia daraja kubwa la uongozi Novemba 05, 1985 alipochaguliwa kuwa Rais.

Mwaka 1933, Mwinyi akiwa na umri wa miaka minane, aliandikishwa kuanza masomo, Shule ya Msingi Mangapwani, Unguja, Zanzibar. Alisoma hapo darasa la kwanza mpaka la nne, alilohitimu mwaka 1936. Alipomaliza darasa la nne, Mwinyi alijiunga na Shule ya kati (middle school), katika Shule ya Dole. Alisoma darasa la tano mpaka la nane mwaka 1942.

Mwaka 1943, Mwinyi alijiunga na Chuo cha Ualimu Zanzibar, aliposoma ngazi ya cheti. Alitunukiwa Astashahada ya ualimu mwaka 1944. Mwinyi alijiendeleza zaidi kwenye fani ya ualimu kwa kusoma Astashahada Kuu ya Ualimu (General Certificate in Education ‘GCE’), kisha Stashahada ya ualimu, kupitia Chuo Kikuu cha Durban, Uingereza.

No comments:

Powered by Blogger.