LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wadau wasisitiza umuhimu wa matumizi salama ya mtandao kuelekea chaguzi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wadau wa teknolojia ya kimtandao mwishoni mwa wiki waliadhimisha Siku ya Usalama Mtandaoni kwa kufanya majadiliano yenye lengo la kukabiliana na upotoshaji na taarifa za uzushi hususani nyakati za uchaguzi.

Akifungua maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam, Rachel Magege ambaye ni Afisa Programu kutoka Shirika la POLLICY alisema lengo la maadhimisho hayo ni kujadili changamoto za data na teknolojia hususani tunapoelekea kwenye uchaguzi na kusisitiza kuwa suala la uadilifu na data ni mambo muhimu.

Kwa upande wake mwasilishaji kutoka Kenya, Muthuri Kathure alisema mara nyingi taarifa za upotoshaji na uzushi zimekuwa zikijitokeza sana wakati wa uchaguzi au mabadiliko ya tabia nchi huku matangazo ya baadhi ya bidhaa zisizofaa kwa walaji zikiendelea kurushwa mtandaoni.

Alisema kuwa haki za kimtandao ni mtambuka kwani zinaathiri sekta za umma na sekta binafsi.

“Changamoto kubwa ambayo Afrika tunakutana nayo ni teknolojia kuandaliwa kwingine bila kuzingatia muktadha wa nchi zetu ambapo jamii zetu huwa hazina uwezo wa kufanya maamuzi katika utengenezaji wa teknolojia hiyo na kuishia kuipokea" alisema.

Akichangia mjadala huo, Wakili Philomena Stanslaus alikiri kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa sana kwenye matumizi ya teknolojia ya kidijiti na kutoa mfano wa malipo katika idara nyingi ambapo hufanywa mtandaoni tofauti na miaka iliyopita.

Alisisisiza umuhimu wa wadau kutumia vyombo vya habari ili kuelimisha jamii juu ya matumizi salama ya mitandao na kukwepa taarifa za upotoshaji.

Kwa mjibu wa takwimu za TCRA za mwaka 2021, Tanzania ilikadiriwa kuwa na watumiaji wa intaneti (mtandao) wapatao milioni 29, karibu nusu ya idadi ya watu.
Na Rose Ngunangwa, Dar

No comments:

Powered by Blogger.