LIVE STREAM ADS

Header Ads

DED Mwanza ataka watendaji kulipwa fedha za ofisi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo.

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetakiwa kutenga na kutoa fedha za uendeshaji ofisi za Kata hatua itakayosaidia kuondokana na adha iliyopo hususani kwa watendaji wakati wakitimiza majukumu yao.

Akihoji swali la papo kwa hapo, Diwani wa Kata ya Isamilo Charles Nyamasiriri aliyehoji "ni lini Watendaji wa Kata watapelekewa fedha ili waondokane na adha waliyonayo ya madeni hususani kwenye steshenali?".

Hayo yalijiri Machi 12, 2024 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kilicholenga pia kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji za Kamati mbalimbali katika kipindi cha robo ya pili mwaka wa fedha 2023/2024.

Nyamasiriri alisema fedha za matumizi ya ofisi zinatakiwa zitolewe kila mwezi na kila Kata inatakiwa ipewe laki tano.

"Mara ya mwisho Ofisi zetu za Kata zilipelekewa fedha mwaka jana mwezi wa tatu hadi sasa tuna mwaka mzima bila kupewa fedha za matumizi ya ofisi, watendaji wa Kata wanapata wakati magumu wa kutekeleza majukumu yao" alisema Nyamasiriri.

Akijibu hoja hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba ambaye amehamia katika Halmashauri hiyo akitokea Manispaa ya Ilemela kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema fedha hizo zinapaswa kupelekwa mara moja katika ofisi za Kata.

"Japo sijachungulia kwenye chungu kuna nini kwa sababu bado sijakabidhiwa rasmi ofisi, lakini hizo pesa zinapaswa kupelekwa kwenye kila Kata na hadi kufikia Ijumaa ziwe zimesoma huko" alisema Kibamba.

Kibamba alisema kiasi cha shilingi milioni tisa zinapaswa kupelekwa katika Kata zote 18 za Jiji la Mwanza kila mwezi ambayo ni sawa na shilingi laki Tano kwa kila Kata na hivyo kumwagiza Mweka Hazina wa Jiji la Mwanza kushughulikia suala hilo.

Kwa upande wake Mweka Hazina wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Edwini Magere alisema maelekezo yaliyotolewa na Mkurugenzi yatatekelezwa mara moja.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sima Constantine Sima akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo.
Diwani wa Kata ya Isamilo, Charles Nyamasiriri akiuliza swali la papo kwa hapo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Jiji la Mwanza.
Baadhi ya madiwani wa Jiji la Mwanza wakisoma taarifa mbalimbali.

No comments:

Powered by Blogger.