LIVE STREAM ADS

Header Ads

DSE ring the bell 2024 yafana

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.comMkurugenzi wa Uwekezaji ndani ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji Aristides Mbwasi (wa tatu kushoto) ambaye alimuwakilisha Waziri wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa mgeni rasmi, akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa yaliyofanyika Machi 8, 2028 jijini Dar es Salaam.

Godwin Myovela, Dar es Salaam
Maelfu ya wanawake nchini jana wamejitokeza kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake (8 Machi 2024) huku Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikitumia siku hii vilivyo kufanya tathmini ya hali ya usawa wa kijinsia, sambamba na kuongeza hamasa juu ya uelewa wa pamoja wa dhana hiyo kupitia mpango wa ‘Ring the Bell for Gender Equality’ (piga kengele kwa usawa wa kijinsia).

Mlio huo wa kengele wa kimataifa, ikiwemo Tanzania, unalenga kuleta umakini kwa jukumu muhimu ambalo taasisi na makampuni mbalimbali zinaweza kutekeleza katika kukuza dhana ya usawa wa kijinsia, ili kutimiza matakwa ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, sambamba na kuongeza ufahamu wa Kanuni za Uwezeshaji Wanawake (WEPs).

DSE imekuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango wa ‘Ring the Bell’ kwa kushirikiana na UN Global Compact Network Tanzania, UN Women, International Finance Corporation (IFC) na Shirikisho la Soko la Dunia, kwa azma ya kukuza dhana ya usawa wa kijinsia katika nyanja zote.

Akizungumza katika hafla hiyo jijini hapa, iliyobebwa na kaulimbiu “Wekeza kwa Wanawake: Kuharakisha Maendeleo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Mary Mniwasa, alisema kuwekeza kwa wanawake katika nyanja mbalimbali kusichukuliwe kama ni jukumu la kijamii pekee; bali ni uwekezaji thabiti wa kibiashara wenye busara.

Mniwasa alisema utafiti unaonesha taasisi na kampuni nyingi ambazo zimejumuisha wanawake kwenye timu zao za uongozi huibuka kidedea kwa kuwashinda wenzao katika masuala ya ubunifu, faida na uendelevu, hivyo kwa kutumia talanta na mitazamo ya wanawake, dirisha la fursa mpya mbalimbali linafunguka-na hatimaye kupelekea ukuaji na uvumbuzi ambao unanufaisha sio tu wenye hisa bali jamii.

“Leo tunapotafakari hatua tulizopiga kuelekea usawa wa kijinsia pia tunapaswa kutambua kazi ambayo bado ipo mbele yetu. Bado wanawake wanaendelea kukabiliwa na vikwazo katika kupata mitaji, nafasi za uongozi na fursa sawa katika sehemu za kazi..ni muhimu kuongeza juhudi ili kusawazisha na kuunda mazingira ambayo kila mwanamke anaweza kustawi na kufanikiwa,” alisema Mniwasa na kuongeza:

Kama viongozi katika sekta za fedha na maeneo mengine, bado tuna fursa za kipekee na wajibu wa kuleta mabadiliko, hususani kwa kuwekeza katika mipango inayosaidia wajasiriamali wanawake, sanjari na kuhamasisha masuala ya usawa wa kijinsia kupitia vikao vya bodi mbalimbali za maamuzi, ili kwa pamoja tuweze kufikia mustakabali wenye mafanikio, jumuishi na endelevu kwa wote.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji ndani ya wizara hiyo Aristides Mbwasi, alisema lengo la Maendeleo Endelevu (SDG 5) na kipaumbele mtambuka katika ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030 ni kufikia usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake na wasichana wote.

Alisema bado kuna baadhi ya wanawake wananyimwa fursa ya kupata huduma za afya, wanakabiliana na vikwazo vya elimu na wengine wapo katika hatari ya kubaguliwa kwenye nyanja za kisiasa na kiuchumi, na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

”Kwa kuzingatia ajenda tuliyonayo ya maendeleo endelevu tunayo fursa ya kusahihisha makosa haya na kutanguliza afya, elimu, haki na ustawi wa wasichana na wanawake kila mahali…na msukumo huu wa usawa unapaswa kutambuliwa sio tu kama haki ya binadamu lakini kama msukumo wa maendeleo,” alisema. Maadhimisho hayo yakiendelea.
Picha zikipigwa wakati wa maadhimisho hayo.
Wadau mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Baadhi ya wadau wakiwa katika picha ya pamoja na waandaaji wa maadhimisho hayo.

No comments:

Powered by Blogger.