LIVE STREAM ADS

Header Ads

Dkt. Biteko ashiriki Misa ya kumuombea Hayati Magufuli

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameshiriki misa takatifu ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Misa hiyo imefanyika Jumapili Machi 17, 2024 katika Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi Mlimani, Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Wilaya ya Chato mkoani Geita.

"Kama alikuwa na mapungufu Mungu amsamehe na kumkaribisha katika ufalme wa mbinguni maana huenda yeye kama binadamu kuna mahali alikosea" amesema Makamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Padri Ovan Mwenge wakati akiongoza ibada hiyo.

"Siyo kazi yetu kuhukumu, kazi yetu ni kumuombea, kama kuna watu hawaamini katika kumuombea marehemu, wabaki hivyo hivyo na kama kuna watu wanaamini basi siku moja tutakutana" amesema Padri Mwenge.

Akitoa salamu kwenye Misa hiyo, Dkt. Biteko ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Hayati Dkt. Magufuli alikuwa na ndoto ya kuwaunganisha watanzania kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo na sasa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendeleza miradi hiyo.

"Dkt. Samia ameendeleza ujenzi wa bwawa la umeme la Mwl. Julius Nyerere, reli ya kisasa ambayo majaribio yamefanyika kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro pamoja na ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi ambalo limefikia zaidi ya asilimia 80 likiunganisha mikoa ya Geita na Mwanza, nataka niwahakikishie hakuna kitakachosimama" amesema Dkt. Biteko.

"Rais wetu Dkt. Samia aliposema Kazi Iendelee alikusudia kuyaendeleza yale yote yaliyobuniwa na Hayati Dkt. Magufuli na nataka niwahakikishie kwamba yote aliyoyaanzisha Rais wetu atayaendeleza kwa kasi kubwa ili watanzania wayapate kama walivyoyakusudia kwa Hayati Magufuli" amesema Dkt. Biteko.

Akiwasilisha salamu za familia, mtoto wa Hayati Magufuli, Jesca Magufuli amesema Hayati Dkt. Magufuli alikuwa mpendwa maendeleo na aliyetanguliza mbele maslahi ya nchi hivyo ataendelea kukumbukwa. Jesca mmeishukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa karibu na familia ya Hayati Magufuli.

Naye mjane wa Hayati Magufuli, mama Janeth Magufuli amewashukuru viongozi wa dini na Serikali kwa jinsi wanavyoshirikiana na familia ya Hayati Magufuli na kuyaenzi yale yote ambayo alikusudia kuyatenda.

"Hayati Dkt. Magufuli yuko kwenye mioyo yetu, daima tutamkumbuka" amesema mama Janeth Magufuli.

Misa hiyo pia imeambatana na kumbukizi ya miaka mitatu tangu kifo cha Dkt. Magufuli (kilichotokea Machi 17, 2021) iliyofanyika katika nyumbani kwake ambayo imehudhuriwa na wanafamilia wakiongozwa na mke wa Hayati Dkt. Magufuli mama Janeth Magufuli, wananchi, viongozi wa dini na Serikali.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kushoto) akiwasili katika kanisa la Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi Mlimani, Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara kuhudhuria misa takatifu ya kumuombea Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
Makamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Padri Ovan Mwenge (katikati) akiongoza misa ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
Waumini wakiwa kwenye Misa ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kushoto) na mjane wa Hayati Dkt John Pombe Magufuli, mama Janeth Magufuli (kulia) wakiwa kwenye Misa hiyo.
Mmoja wa wanafamilia, Jesca Magufuli akiwa kwenye misa hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.