LIVE STREAM ADS

Header Ads

Nyamagana wapanda miti kuelekea Siku ya Wanawake Duniani 2024

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayofayika Machi 08 kila mwaka, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza imetumia fursa hiyo kupanda miti zaidi ya 3000 katika shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuendelea kutunza mazingira.

Zoezi hilo limefanyika Machi 04, 2024 katika shule ya msingi Kishiri, shule za sekondari Fumagila na Sahwa jijini Mwanza.

Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi amesema wamepokea aina mbalimbali za miche ya miti kutoka kwa Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania (TFS) ikiwemo ya matunda, mbao na kimvuli na kuipanda katika taasisi za Serikali ili kuendelea kuifanya Nyamagana kuwa ya kijani.

"Tunapanda miti ili itutunze sisi na kizazi chetu kijacho, pia itatusaidia kupata mvua za kutosha, tutapunguza hewa ya ukaa, tutaondokana na ukame na watoto wetu watapata lishe bora kupitia miti ya matunda na hivyo kuepukana na utapiamlo" amesema Makilagi.

Aidha alitoa wito kwa walimu pamoja na wanafunzi kuituza miti hiyo ili iwe na tija kwa jamii na kudumisha uoto wa asili kuanzia kwenye makazi, taasisi na maeneo ya wazi.

Kwa upande wake Diwani Viti Maalum Kata ya Kishiri, Magreth Kuhanwa ameahidi kusimamia miti hiyo ili ikue vizuri ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuimwagilia pindi mvua zitakapokata.

Amesema wataendelea kuelimisha na kuhamisha jamii ili kila mmoja aone umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kishiri, Mwl. Frank Swanka ameahidi kushirikiana na walimu wenzake pamoja na wanafunzi katika kuhakikisha miti hiyo inakua na kuweka mazingira ya kuvutia shuleni hapo.

Naye Afisa Mistu kutoka TFS Wilaya ya Nyamagana, Sharifa Kayoza amesema taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinajitoleza kwa wingi kuchukua miti kwa ajili ya kupanda na hivyo tunawaomba wawe na utaratibu mzuri wa kuitunza ili wazidi kuboresha mazingira.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo "Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii".
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Afisa Mistu TFS Wilaya ya Nyamagana, Sharifa Kayoza (kushoto) akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti lililofanyika jijini Mwanza.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Kishiri jijini Mwanza, Anneth Jonathani akishiriki zoezi la kupata miti kuelekea siku ya wanawake duniani 2024.

No comments:

Powered by Blogger.