LIVE STREAM ADS

Header Ads

Viongozi wa Serikali watakiwa kufanikisha ujenzi wa minara ya mawasiliano

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Viongozi na watendaji mbalimbali wa Serikali wametakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa vibali vya ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu ili kufikisha huduma hiyo kwa wananchi.

Rais hiyo imetolewa Aprili 23, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala wakati akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Said Mtanda kwenye uzinduzi wa kampeni ya elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ya simu nchini.

Masala amesema lengo la Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ni kuwezesha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu na data hadi ya vijijini kwa kutoa ruzuku ya ujenzi wa minara hivyo viongozi wanao wajibu wa kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri katika utekelezaji wa mradi huo.

Aidha Masala ametoa rai kwa shirika la TANESCO/ REA kufikisha huduma ya nishati ya umeme katika maeneo ambapo ujenzi wa minara hiyo unafanyika huku TANROADS/ TARURA nao wakihakikisha miundombinu ya barabara inapitika ili kufikisha vifaa vya ujenzi.

Masala ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya mawasiliano ambayo itasaidia wananchi taarifa na huduma ya mawasiliano na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi.

Naye Mratibu wa UCSAF Kanda ya Ziwa, Mhandisi Bernard Buremo amesema mradi wa ujenzi wa minara 758 ulisainiwa Mei 13, 2023 ambapo hadi kufikia Mei 02, 2025 minara hiyo inapaswa kuwa imekamilika.

Ametaka makampuni ya mawasiliano yaliyonufaika na ruzuku kutoka UCSAF kuwa ni Airtel (minara 169),  TTCL (minara 104), Tigo (minara 261), Halotel (minara 34) na Vodacom (minara 190) ambapo jumla ya ruzuku kwa minara 758 ni shilingi bilioni 126.

"Mkoa wa Mwanza pekee umepata minara 16 itakayonufaisha vijiji 52 vyenye wakazi 296,410 ambapo ruzuku iliyotolewa ni shilingi bilioni 2.4" amesema Mhandisi Buremo.

Mhandisi Buremo ameongeza kuwa tayari ujenzi wa minara 103 imekamilika na kuanza kutoa huduma ya mawasiliano katika mikoa mbalimbali nchini ambapo Airtel imewasha minara 61, Vodacom minara tisa, Halotel nane na Tigo minara 25 na kwamba hadi sasa UCSAF imesaidia huduma ya mawasiliano ya simu kufikia asilimia 98 ya watanzania ikilinganishwa na asilimia 48 mwaka 2006 kabla mfuko huo haujaanza kufanya kazi.

Afisa Habari UCSAF, Celina Mwakabwale amesema mfuko huo umejikita kutoa ruzuku kwa watoa huduma ili kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo hasa vijijini ambapo ujenzi wa mnara mmoja hugharimu zaidi ya shilingi milioni 300.

Afisa Tarafa ya Mumbuga wilayani Ukerewe, Josephat Mazula amesema mradi huo utasaidia kuondoa changamoto ya ukosefu wa mawasiliano ya simu vijijini kwani mawasiliano ya uhakika ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Said Mtanda wakati wa uzinduzi wa kampeni ya elimu kwa umma Kanda ya Ziwa kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ya simu Tanzania Bara. Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika Aprili 23, 2024 jijini Mwanza kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao unatoa ruzuku kwa makampuni ya simu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Said Mtanda wakati wa uzinduzi wa kampeni ya elimu kwa umma Kanda ya Ziwa kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ya simu Tanzania Bara.
Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali Watu na Utawala Mkoa Mwanza, Daniel Machunda akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya.
Mratibu wa UCSAF Kanda ya Ziwa, Mhandisi Bernard Buremo akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.
Afisa Habari UCSAF, Celina Mwakabwale akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.
Viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya mkoani Mwanza wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi wa kampeni ya utoaji elimu kwa umma Kanda ya Ziwa kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ya simu Tanzania Bara umehudhuliwa na viongozi wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri, Watendaji wa Kata na Tarafa ili kuwajengea uelewa wa kusaidia utekelezaji wa mradi huo katika maeneo yao ikiwemo kusaidia upatikanaji wa vibali.
Mnara wa mawasiliano ya simu.
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.