LIVE STREAM ADS

Header Ads

Marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje kukidhi mahitaji ya watanzania

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk amesema marekebisho ya Sera ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharibi ya mwaka 2001 iliyoanza kutumika mwaka 2004 yatasaidia upatikanaji wa Sera bora itakayoeandana na wakati na hivyo kukidhi mahitaji ya sasa ya wananchi.

Balozi Mbarouk aliyasema hayo jijini Mwanza wakati akizungumza kwenye kongamano la wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera hiyo na kuongeza kuwa maoni yanayotolewa na watanzania yatasaidia kupata Sera itakayochochea maendeleo nchini.

“Sera iliyopo haitoi majawabu ya changamoto za kimaendeleo, kwa mfano kuna watanzania wako nje ya nchi na wangependa kushiriki kwenye shughuli za kimaendeleo katika nchi yao, marekebisho haya yanakwenda kutoa fursa hiyo” alisema Balozi Mbarouk.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa alisema hatua ya kukusanya maoni kwa ajili ya marekebisho ya sera hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alitaka kupatikana kwa Sera iliyowashirikisha watanzania walio wengi baada ya wataalamu kumaliza kazi yao na kwamba marekebisho hayo yatagusa nyanja mbalimbali ikiwemo diplomasia ya uchumi.

Naye Mkuu wa Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alisema ni muhimu wananchi kuendelea kutoa maoni ili kupata sera itakayochochea fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi akitolea mfano Mkoa Mwanza ambao ni kitovu cha nchi za Afrika Mashariki.

Baadhi ya wadau kwenye kongamano hilo akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la KIVULINI, Yassin Ally alisema ni vyema Serikali kuweka mkakati wa kufanya marekebisho ya sera mbalimbali kila baada ya miaka mitano ili kuendana na mahitaji ya wakati husika tofauti na sasa ambapo sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001 inafanyiwa marekebisho baada ya miaka 23.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa Mwanza, Masala Kulangwa alisema marekebisho ya sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001 hayapaswi kujumuisha suala la uraia pacha kwani watanzania wanapaswa kujivutia Taifa lao wanapokuwa nje ya nchi.

Tayari Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekusanya maoni ya wananchi kuhusu marekebisho ya Sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001 katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Unguja na Pemba na inaendelea na zoezi hilo.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza kwenye kongamano la wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 lililofanyika jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza kwenye kongamano la wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 lililofanyika jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akizungumza kwenye kongamano la wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 lililofanyika jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akizungumza kwenye kongamano la wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 lililofanyika jijini Mwanza.
Mkuu wa Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda (hayuko pichani) kwenye kongamano hilo.
Wadau akiwemo Mkurugenzi wa shirika la KIVULINI, Yassin Ally (katikati) wakifuatilia kongamano la wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 lililofanyika jijini Mwanza.
Wadau akiwemo Mwenyekiti wa Wazee Mkoa Mwanza, Masala Kulangwa (kushoto) wakifuatilia kongamano hilo.
Wadau mbalimbali wakifuatilia kongamano kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 lililofanyika jijini Mwanza.
Kongamano hilo lilihusisha makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, siasa, machinga, watu wenye ulemavu, serikali, mashirima binafsi na wajasiriamali/ machinga.

No comments:

Powered by Blogger.