LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mwekezaji wa nguruwe atoa ahadi kila la Simba SC

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi wa kampuni ya Kijiji cha Nguruwe Project kilichopo Zamahero wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma ambaye ni shabiki kindakindaki wa Timu ya Simba SC Simon Mnkondya ameahidi kutoa zawadi ya Nguruwe mmoja mkubwa aina ya Large White mwenye kilo 500 sawa na shilingi Milioni 3 kwa kila goli litakalofungwa na Simba SC katika mchezo wake na Ihefu SC kesho Jumamosi Aprili 13,2024 katika uwanja wa Iliti Singida.

Ahadi hiyo ya Mkondya ambaye ni mdau mkubwa wa michezo imekuja siku chache tu baada ya juzi kutoa ahadi ya kuwapa Dodoma Jiji Nguruwe ama shilingi laki saba kwa kila goli ambalo wangelifunga dhidi ya Yanga Sc lakini bahati mbaya hawakufunga hivyo kukosa zawadi hiyo.

"Juzi nilitoa ahadi ya kuwapa Dodoma Jiji Nguruwe mwenye thamani ya shilingi laki saba kwa kila goli ambalo wangelifunga dhidi ya Yanga SC, bahati mbaya hawakufunga na hivyo kukosa zawadi hiyo nawapa pole sana.

Sasa mimi pia ni shabiki wa timu ya Simba Sports Club, na timu yetu kwa sasa inapitia wakati wa ngumu wa upatikanaji matokeo tumefungwa mechi tatu mfululizo na Al Ahly nje ndani na kutolewa katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, pia tukafungwa na Mashujaa na kutolewa katika michuano ya Shirikisho Tanzania hii ni aibu kwetu" amesema Mnkondya.

"Sasa ili kuwapa motisha katika mchezo wa kesho dhidi ya Ihefu SC ama kama inavyofahamika sasa kama Singida Black Stars mimi na Kampuni yangu tunaahidi kutoa Nguruwe mmoja mkubwa aina ya Large White mwenye kilo 500 kwa kila goli litakalofungwa na Simba katika mchezo huo au kiasi cha shilingi milioni tatu ambayo ni thamani ya Nguruwe huyo.

Lakini pale Simba kuna watu wawili wanafanya kazi sana na hao napenda kuwapa zawadi ya nguruwe kama tutashinda mchezo wa kesho ambao ni msemaji Ahmed Ally na mchezaji Clatous Chama, hawa wanapambana sana" amesema Mnkondya.

Mradi wa Kijiji cha Nguruwe upo Zamahero Dodoma Zamahero, ambapo watu mbalimbali wamekuwa wakifika hapo kuwekeza ili kuinua uchumi, michezo nk.

Uongozi wa Simba umebainisha kuwa matokeo ambayo wanayapata yanaumiza kwelikweli kwa kuwa ni mabaya ndani ya muda mfupi.

Ipo wazi kwamba Aprili 06 2024 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali baada ya dakika 90 ubao ulisoma Al Ahly 2-0 Simba.

Kwenye mechi mbili za kimataifa Simba imefungwa mabao matatu huku safu yao ya ushambuliaji ikikwama kufunga hata bao kwa wapinzani wao.

Wakarejea tena Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma ubao ukasoma Mashujaa 1-1 Simba walipofika katika changamoto ya penalti ilikuwa Mashujaa 6-5 Simba ilikuwa ni Aprili 9 2024.

Ndani ya siku tatu Simba imefungashiwa virago katika mashindano mawili makubwa, Ligi ya Mabingwa Afrika na CRDB Federation Cup.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema: “Inaumiza kwa kweli matokeo ambayo tunayapata. Kupata matokeo mabaya ndani ya siku tatu inaumiza kwelikweli”.




Kituo kinachofuata ni Aprili 13 dhidi ya Ihefu, Uwanja wa Liti ambapo Simba itakuwa ugenini.

No comments:

Powered by Blogger.