Wadau wa Bima Kanda ya Ziwa wapewa elimu, msisitizo watolewa kwa wakulima
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware akizungumza kwenye mkutano wa kutoa elimu ya bima na kupokea maoni kutoka kwa wadau Kanda ya Ziwa uliofanyika jijini Mwanza.
Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Richard Toyota akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa bima uliofanyika jijini Mwanza.
Wadau wa bima Kanda ya ziwa wakifuatilia mada mbalimbali kwenye mkutano wa wadau wa bima uliofanyika jijini Mwanza.
Wadau wa bima Kanda ya ziwa wakiwa kwenye mkutano huo.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware amewahimiza wakulima kujiunga na huduma za bima za kilimo kwa ajili ya kujikinga na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko, ukame na wadudu waharibifu.
Dkt. Saqware amesema hayo Jumatano Aprili 17, 2024 kwenye mkutano wa kutoa elimu ya bima na kupokea maoni kutoka kwa wadau wa bima Kanda ya Ziwa uliofanyika katika Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza.
Amesema wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara ikiwemo kuporomoka kiuchumi kutokana na kukosa bima ambayo ingewasaidia kufidia hasara mbalimbali wanazozipata pindi majanga yanapotokea.
"Faida za kutumia bima ni nyingi kwenye maisha, inapunguza umasikini, inachochea uchumi na kufanya biashara kuwa endelevu" amesema Dkt. Saqware.
Aidha amesema mpango uliopo ni kutoa elimu kwa watanzania kama ilivyoelekezwa katika mpango wa kuendeleza sekta ya fedha nchini uliyoandaliwa na Wizara ya Fedha ili kuanzia mwaka 2020 hadi 2030, asilimia 80 ya watanzania wawe na elimu ya bima na asilimia 50 wajiunge na bidhaa za bima kutoka kwa watoa huduma ambao wamepewa leseni na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
Naye Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Ziwa, Richard Toyota amesema suala la uelewa wa bima bado liko chini kwani ni asilimia 15 ya watanzania ndio wana uelewa wa bima huku mchango wa Kanda ya Ziwa kwenye pato la bima kitaifa ukiwa ni asilimia nne.
"Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ina zaidi ya watu milioni 16, kama mchango wetu ni asilimia nne kwenye pato la Taifa la bima, bado ni kiwango kidogo ukilinganisha na idadi ya watu" amesema Toyota akieleza umuhimu wa Elimu ya bima kuendelea kutolewa kwa wananchi.
Mmoja wa wadau wa bima kwenye mkutano huo ambaye ni Afisa Bima kutoka Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kanda ya Ziwa, Vincent Mushi amesema mazao waliyoyaweka kwenye bima kwa mwaka huu 2024 ni mahindi, maharage, mpunga, korosho, pamba na alizeti hivyo mteja anapopata hasara shirika litamfidia.
Mshiriki mwingine aliyeshiriki mkutano huo ambaye ni Mariam Meghji ameomba elimu ya bima kuendelea kutoelewa hususani kwa makundi ya Vijijini wakiwemo wakulima hiyo ili kutambua umuhimu wa kujiunga na bima na kuepuka hasara wanayoweza kupata wakati wa majanga.
No comments: