LIVE STREAM ADS

Header Ads

Taasisi ya 'Peace For Conservation' yakabidhi baiskeli kwa wahitaji Busega, Simiyu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Taasisi ya Uhifadhi wa Wanyamapori 'Peace For Conservation- PFC' imetoa msaada wa baiskeli (viti mwendo), kwa watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto ya kutoweza kutembea.

Zoezi la kukabidhi baiskeli hizo limefanyika Ijumaa Mei 10, 2024 huku wanufaika wakiwa ni wazee, wanawake na watoto ambao wanatoka katika familia duni kiuchumi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Davis Kabambo alisema msaada wa baiskeli hizo utawasaidia kuondokana na changamoto ya kukaa ndani muda mrefu wanapokosa mtu wa kuwasaidia kutoka nje.

"Baadhi tumekuta wamekaa ndani muda wote, wakisema wanafamilia wanapoenda kwenye shughuli za kilimo, wanakosa mtu wa kuwatoa ama kuwaingiza ndani hivyo baiskeli hizi zitawasaidia kujihudumia" alisema Kabambo.

Mmoja wa walionufaika na msaada huo, mzee Emmanuel Shinji mkazi wa Lamadi alisema amekuwa akikaa ndani kwa muda wa miaka minne kutokana na mke wake kutomudu kumtoa nje mwenyewe kulingana na uzito alionao.

"Nimeishi na huyu mama kwa upendo mkubwa tangu nilipopata ulemavu, nawashukuru kwa msaada huu, leo nimetoka nje na kuona jua" alisema Shinji.

Mke wa mzee Shinji, Kezia Maduhu alisema kupitia baiskeli, sasa ataweza kumhudumia kwa urahisi mmewe ambapo alitoa rai kwa taasisi ya PFC kuendelea kuwatambua na kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Kwa muda mrefu, taasisi ya PFC imekuwa ikiwasaidia wakazi wanaozunguka hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na Pori la Akiba la Kijereshi ambapo kwa mwaka huu imekabidhi baiskeli 11 kwa watu wenye ulemavu zikiwa na thamani ya shilingi milioni tatu na laki tatu.

Pia taasisi hiyo imekuwa ikiwasaidia vijana kupitia michezo kwa kuanzisha mashindano mpira ya vijiji na shule yaitwayo 'Rhino Cup Champions League'. 

Shule inayoibuka na ubingwa hunufaika na ujenzi wa miundombinu ikiwemo vyoo na madarasa huku upande wa vijiji, zawadi mbalimbali hutolewa ambapo lengo ni kuendeleza wachezaji wenye vipaji badala ya kuangukia kwenye uwindani haramu kuzunguka hifadhi za wanyama. 
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Peace For Conservation, David Kabambo (kushoto aliyesimama) akimkabidhi baiskeli mzee Emmanuel Shinji mkazi wa Lukungu. Anayeshuhudia kulia ni Mtendaji Kata ya Lamadi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Peace For Conservation, David Kabambo akimbeba bibi mwenye ulemavu, Rejina Maduhu mkazi wa Kijiji cha Kabita wilayani Busega wakazi wa zoezi la kumkabidhi baikeli (kiti mwendo).
Mmoja wa watoto wenye ulemavu katika Kijiji cha Mwakiloba Mbugani, Lucy Mashaka (aliyekaa chini) na familia yake wakimlaki kwa furasa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Peace For Conservation, David Kabambo alipofika nyumbani kwao kumkabidhi baikeli.

No comments:

Powered by Blogger.