Wenye ulemavu waomba nafasi kwenye miradi ya kiuchumi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Ombi hilo lilitolewa Mei 18, 2024 na Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Wilaya ya Nyamagana, Hamza Nyamakurura kwenye kongamano la uchumi kwa watu wenye ulemavu lenye lengo la kuhakikisha kunakuwepo na utekelezaji wa haki za kazi na ajira kwa watu wenye ulemavu lililofanyika jijini Mwanza.
Alisema watu wenye ulemavu wanapata changamoto kupata maeneo ya kufanyia shughuli za uzalishaji mali hivyo mradi wa Soko Kuu jijini Mwanza utakapokamilika wanaomba kupata nafasi katika eneo hilo hatua itakayosaidia kukuza fursa ya uchumi wao.
"Kongamano hili kinakaulimbiu isemayo 'atutaki ombaomba, tunataka kazi'. Hii ina maana kazi inamwezesha binadamu kujitegemea na kupata heshima katika jamii hivyo tunaomba Serikali iweze kusikia ombi letu" alisema Nyamakurura.
Akitoa mada ya haki ya kazi na ajira kwa watu wenye ulemavu, Wakili wa kujitegemea, Remigius Mainde alisema Sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 ibara ya 33, ibara ndogo ya tatu inasema kila mwajiri anaeweza kuajiri watu 20 ni lazima asilimia tatu wawe watu wenye ulemavu na atengeneze miundombinu itakayowawezesha kufanya kazi.
Alisema pamoja na kuwepo kwa Sheria hiyo, bado kuna baadhi ya waajiri hawafuati utaratibu hivyo Serikali inatakiwa kutengeneza mfumo utakaohakikisha Sheria hiyo haivunjwi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu, Kaazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Godfrey Chambu alisema kwa sasa wanafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 ili iendane na mazingira ya sasa.
Naye Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake na Watoto Chama cha Walemavu wa Viungo Tanzania (CHAWATA), Janeth Maila alisema kwenye suala la ajira wamekuwa wakibaguliwa jambo ambalo limekuwa likiwaathili kisaikolojia.
"Tunashukuru leo kukutana kwenye kongamano hili ambalo litatusaidia kukuza na kuongeza ufahamu kwa watu wenye ulemavu" alisema Maila.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala alitoa rai kwa watu wenye ulemavu kuzingatia taratibu na maagizo yanayotolewa katika uombaji wa ajira zinapokuwa zimetangazwa.
"Katika kuhakikisha suala la ajira kwa watu wenye ulemavu linapewa kipaumbele, Serikali imeendelea kutoa nafasi za ajira kwa watu wenye ulemavu ambao wanakidhi vigezo na wenye sifa. Serikali imeweka msisitizo kwa mwombaji kujieleza uleumavu alionao ili kurahisisha uchambuaji wa maombi ya kazi lakini suala hili bado linekosa uwazi na kusababisha changamoto kwa baadhi ya waombaji kukosa nafasi" alisema Masala.


Na Hellen Mtereko, Mwanza
No comments: